30 July 2012
Wateja wa TANESCO wasikilizwa
Na Benedict Kaguo, Dodoma
SERIKALI imepunguza gharama za kuunganisha umeme ambapo kuanzia Januari 2013, wateja ambao watataka kuvutiwa umeme na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), watalipia sh. 177,000, badala ya sh. 455,000 wanazolipia sasa.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba ya Wizara yake na kuongeza kuwa, gharama hizo zitawawezesha wananchi wengi kuvuta umeme.
Alisema wateja ambao wataunganishiwa umeme kutoka umbali usiozidi mita 30 bila hitaji la nguzo katika maeneo ya vijijini, watalipa sh. 177,000 ambapo wale wa mijini sh. 320,960 badala ya sh. 455,108 zinazolipwa na wateja kwa sasa.
“Punguzo hili ni sawa na asilimia 68.11 kwa wateja waishio vijijini na 29.48 kwa wateja wa mijini lakini wateja ambao watajengewa njia moja na kuwekewa nguzo moja kwa upande wa vijijini watalipa sh. 337,740 na mijini sh.515,618 badala ya sh. milioni 1,351,884 zinazolipwa sasa sawa na punguzo la asilimia 75.02 vijijini na asilimia 61.86 mijini.
Alisema wateja ambao watajengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili maeneo ya vijijini watalipa sh. 454,654 na mijini sh. 696,670 badala y sh. milioni 2,001,422 zinazolipwa sasa sawa na punguzo la asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na 65.19 mijini.
Alisema Serikali pia imeanzisha utaratibu wa kugharamia miundombinu ya kufikisha umeme kwa wateja kupitia miradi inayopata ruzuku kutoka Mfuko wa Nishati Vijijini (REF).
Prof. Muhongo alisema utaratibu huo utatumika kwa wateja ambao watakuwa wamefunga nyaya za umeme katika nyumba zao kwenye maeneo ya miradi husika.
“Mpango huu utapunguza gharama za kuunganishiwa umeme kwa wastani wa asilimia 80, kulingana na idadi ya nguzo na mfumo utakaotumika, idadi ya wateja wa awali ambao wataunganishiwa umeme kupitia mpango huo ni 100,000,” alisema.
Aliongeza kuwa, Serikali katika kutekeleza jukumu lake la kusimamia taasisi zilizo chini yake, imegundua kuwa TANESCO inakabiliwa na changamoto kubwa ya upotevu wa umeme wa kiufundi na usio wa kiufundi unaokadiriwa kufikia asilimia 21.
Alisema Wizara pia imegundua sehemu kubwa ya upotevu wa umeme usiokuwa wa kiufundi, unasababishwa na wizi unaofanywa na wananchi kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo wasio waaminifu na mafundi wa mitaani 'vishoka'.
Aliongeza kuwa, mwaka 2011/12 Serikali kupitia shirika hilo imechukua hatua mbalimbali za kinidhamu zikiwemo kuwafukuza kazi watumishi 17, kuwafikisha watumishi saba maahkamani na kung'oa mindombinu iliyojengwa na vishoka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

Nimeipenda sana Bajeti hii ya Wizara. Huyu Waziri ni Mzalendo kabisa. Anaelewa maisha ya watu yalivyo, hasa kijinini. Ila Itachukua muda gani kuunganishiwa na utekelezaji unaanza lini. Nataka niende kijijini kwetu nikafanye miradi yangu.
ReplyDelete