30 July 2012

John Komba afanyiwa upasuaji



Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Mbinga Magharibi, mkoani Ruvuma, Bw. John Komba amefanyiwa upasuaji wa nyonga nchini India ambayo ilikuwa ikimsumbua katika mguu wa kulia.

Bw. Komba ambaye amerejea nchini jana, amedai kusikitishwa na taarifa zinazodai alikuwa mahututi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Komba alisema upasuaji huo amefanyiwa katika Hospitali ya Appolo iliyopo Hydrabad, mwanzoni mwa Julai mwaka huu.

Alisema aliondoka Dar es Salaam kwenda India Julai 2 mwaka huu, baada ya kushindwa kupatiwa matibabu nchini kutokana na mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea.

“Siku niliyopelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), tayari madaktari walikuwa wameanza mgomo hivyo niliujulisha uongozi wa Bunge na kumuomba Rais Jakaya Kikwete kwa mamlaka yake anisaidie nikatibiwe nchini India,” alisema Bw. Komba.

Aliongeza kuwa, uzito ulichangia mifupa kusagana kwenye nyonga katika upande wa mguu wa kulia ambapo hadi anakwenda nchini India, alikuwa na uzito wa kilo 138, wakati uzito unaotakiwa kulingana na mwili wake kilo 90 au 100.

“Nimerejea nchini nikiwa na uzito wa kilo 128, ambao nimetakiwa kuudhibiti na kuupunguza kwa kipindi hiki ambacho nitalazimika kupumzika nyumbani kabla ya kuanzia kazi Septemba mwaka huu kama nilivyoelekezwa na madaktari,” alisema.

Akizungumzia upasuaji ulivyofanyika, Bw. Komba alisema ulichukua saa tano hadi kukamilika bila matatizo ambapo sehemu iliyopasuliwa ni ya ukubwa wa futi moja.

Alisema baada ya kufanyiwa upasuaji hakuweza kurejea katika wodi ya kawaida kwa sababu majongwa kadhaa yaliibuka ikiwemo homa kali na presha hivyo alilazimika kulazwa katika wodi ya wagonjwa waliopo kwenye uangalizi maalumu (ICU) kwa siku tano.

“Nimerejea nchini nikiwa mzima, kwa sasa natumia fimbo ili uzito usielemee upande wa kulia nilikofanyiwa upasuaji lakini sijambo kabisa,” alisema Bw. Komba.

Bw. Komba alishangazwa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo viliripoti kuwa anasumbuliwa na figo pia alikuwa mahututi jambo ambalo halina ukweli wowote.

“Si kweli kwamba nilikuwa mahututi, kama kulikuwa na taarifa tofauti ilikuwa jambo rahisi tu, wangekuja nyumbani kuniuliza au kuuliza mke wangu wangepata jibu sahihi,” alisema.


No comments:

Post a Comment