06 July 2012

Wananchi: Tafiti za utawala bora APRM zifanyiwe kazi


Na Mwandishi Wetu

WANANCHI wa kada mbalimbali, wamesema ili kuboresha na kuinua utawala bora nchini, Serikali inapaswa kufanyia kazi tafiti zinazofanywa na taasisi zake kama APRM, hasa zinazohusu suala zima la utawala bora.


Ushauri huo umetolewa Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti na wananchi waliotembelea banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasba), yanayoendelea Barabara ya Kilwa.

Walisema APRM ni Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora nchini ambapo taasisi hiyo imepewa dhamana ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu hali ya utawala bora ili kuisaidia Serikali kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza.

“Tumekuwa tukizisikia taarifa za utafiti wa APRM hasa kuhusu nchi yetu inavyojenga uelewa wa wananchi ili waseme utawala bora wanaoutaka,” alisema mmoja wa wananchi hao.

Baadhi ya wananchi walitaka kueleweshwa jinsi ya kushiriki mchakato huo na wengine wakionesha wasiwasi wao kama taasisi hiyo imetangazwa vya kutosha ili kuwapa nafasi wananchi.

Akifafanua baadhi ya kero za wananchi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas, alisema mchakato huo ulipoanza nchini, wananchi walielimishwa kupitia mikutano iliyofanyika mijini, vijijini, kupitia semina za makundi na vyombo vya habari.

“Kuhusu Serikali kufanyiakazi maoni ya wananchi, kimsingi bado hatujafikia hatua hiyo maana katika mchakato huu, baada ya Rais kuwasilisha ripoti mbele ya wakuu wenzake wa Umoja wa Afrika, anapewa michango alafu nchi inaanza kufanyiakazi maoni ya wananchi kwa miaka mitatu kabla ya kufanyika tena utafiti mwingine,” alisema.

Aliongeza kuwa, kabla ya hatua hiyo kufikiwa nchi haizuiwi kuanza kufanyiakazi maoni ya wananchi wake yaliyotolewa katika ripoti.

“Hapa nchini ukiangalia maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu masuala kama katiba na matakwa ya kudhibitiwa matumizi holela ya fedha katika chaguzi, haya yameshafanyiwa kazi au yanaendelea kufanyiwa kazi, ni sehemu ya maoni ya wengi katika ripoti za APRM,” alisema Bw. Abbas.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 32 za Afrika zinazoshiriki mchakato wa APRM unaolenga kuzipa fursa nchi za Afrika kujitathmini Kiutawala Bora kwa kuwapa nafasi wananchi wao na wataalamu wa ndani kutoa maoni yao ambapo mchakato huo ni endelevu na hurudiwa kila baada ya miaka minne.

No comments:

Post a Comment