06 July 2012

Wadau RLDP waazimia kujiendeleza


Na Rose Itono

WADAU wa Programu ya Kuendeleza Wakulima Vijijini (RLDP), wameazimia kujiendeleza wenyewe katika sekta hiyo ili waweze kujiletea maendeleo endelevu na kujikomboa kiuchumi.

Wakizungumza katika mkutano wa wadau juzi, wadau hao walisema suala la maendeleo linahitaji ushirikiano wa pamoja ili kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo.


“Kimsingi sisi kama wadau tuko tayari kujiendeleza wenyewe baada ya wafadhili kuondoka ili kuchochea maendeleo zaidi, kukuza uchumi wetu na Taifa kwa ujumla,” alisema mshiriki wa mkutano huo Bw. George Mpanduji, kutoka mkoani Shinyanga.

Alisema wafadhili wanapokuja nchini, hawakai muda mrefu hivyo kutokana na hali hiyo, wameamua kuchukua jukumu la kujiendeleza ili waweze kusimamia vyema miradi wanayoachiwa.

Mdau mwingine, Alisia Ngalya, ambaye ni mfugaji wa kuku wa kienyeji kutoka Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma, alisema programmu ambayo inaratibiwa na RLDP, imewasaidia kuinua kipato cha baadhi ya wafugaji wilayani hapo.

“Awali wafugaji wengi hawakuwa na mafunzo ya aina yoyote huvyo kupunguza kipato chao na kuku wengi walikufa ila baada ya mradi huu kuja wilayani kwetu, tumepatiwa mafunzo ya ufugaji bora wa kujiongezea kipato,” alisema.

Meneja mradi wa RLDP, Bw. Francis Massawe, alisema zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo nchini ambazo zinakwamisha juhudi za wakulima kujikomboa kiuchumi.

Aliongeza kuwa, changamoto kubwa ni tatizo la ukame hasa kwenye mikoa ya Kanda ya Kati ambayo imekuwa na upungufu wa mvua ya kutosha katika misimu mingi ya kilimo.

“Ukosefu wa soko la kuuzia mazao mbalimbali, ukosefu wa pembejeo za kilimo pamoja na usindakaji wa hali ya chini katika bidhaa ambazo hazijafikia ubora unaotakiwa katika soko ni tatizo kubwa,” alisema Bw. Massawe.

Alisema pamoja na mambo mengine, washiriki wa mkutano huo wamejadili namna ya kukabiliana na changamoto hasa hizo katika miradi yao mbalimbali ya kilimo.

“Wakulima wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu bila  kujua wanapolima watapa au watakosa, katika mkutano huu pia tumejadili mafanikio yaliyopatikana katika awamu iliyopita na kujipanga katika awamu hii ya mradi,” alisema.

Bw. Massawe aliongeza kuwa, mradi huo ambao ni wa awamu ya nne umeanza tangu Aprili mosi mwaka huu na unatarajiwa kumalizika Machi 2016 ambapo program hiyo inafadhiliwa na Serikali ya Uswisi kupitia Shirika lake la Maendeleo na Ushirikiano (SDC).

Alisema mradi huo unajikita katika sekta ya pamba, alizeti, mpunga, kuku wa kienyeji na programu ya redio kwa wanawake kama njia moja wapo ya kuwafikia watu wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment