10 July 2012

Wana-Yanga Chalinze kukutana leo


Na Elizabeth Mayemba

WANACHAMA wa Yanga tawi la Chalinze wanatarajiwa kukutana leo kwa ajili ya kuzungumzia ajenda mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi mdogo wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.

Akizungumza na Gazeti hili jana, Mwenyekiti wa tawi hilo Adam Kiponzile alisema moja ya ajenda hiyo ni kupokea taarifa kutoka katika kamati ya kutafuta ardhi, kusoma mapato na matumizi na kujadili suala zima la uchaguzi huo na Mkutano Mkuu wa wanachama wote wa klabu hiyo.


"Ni kawaida yetu kuitisha vikao kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo katika klabu yetu, na tunafanya hivi kabla ya kuingia katika uchaguzi mdogo na Mkutano Mkuu," alisema Kiponzile.

Alisema mkutano huo unatarajiwa kuanza saa tisa alasiri na kila mwanachama ataweza kuchangia na tapatiwa maelezo mazuri, ili kila mmoja aweze kujua mambo yanavyokwenda katika klabu hiyo kupitia tawi hilo.

Kiponzile alisema kila mwanachama anatakiwa kufika bila kukosa katika mkutano wa leo, kwani ni haki ya kila mtu na pia ni nafasi nzuri kwa wanachama kuhoji mambo mbalimbali ili kupata ufumbuzi.

Pia Mwenyekiti huyo alisema watatumia fursa hiyo kupitia jina moja moja kwa  wagombea na kuangalia ni yupi atafaa kuingoza klabu yao na si kukurupuka na msimamo wao wote utakuwa ni mmoja.

No comments:

Post a Comment