10 July 2012

Michezo inasaidia kuboresha utendaji kazi'



Na Mwandishi Wetu

BENKI ya Standard Chartered– Tanzania imesema kuwa michezo ni nguzo pekee inayoweza kusaidia kuboresha utendaji kazi ndani ya benki na kukuza mahusiano baina ya wafanyakazi.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Uhusiano wa Benki ya Standard Chartered, Juanita Mramba, wakati wa siku ya michezo mwaka 2012 ya benki hiyo iliyofanyika katika viwanya vya michezo vya Heaven of Peace wikiendi hii.


“Hili ni tukio muhimu kwetu kwa kuwa sisi kama benki ya Standard Chartered tunataka tuendelee kuwepo hapa milele na milele na kwa kupitia michezo tutaweza kuifanya miili yetu kuwa katika afya bora na hivyo kufanyakazi vizuri.

Matukio kama haya yanatusaidia kuzileta familia zetu pamoja, ambapo inatusaidia pia kufahamiana pamoja na kukuza ushirikiano katika kazi,” alisema, Mramba.

Akizungumza wakati michezo hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi, alisema michezo inawasaidia wafanyakazi wa benki yake kuwa na afya bora ambayo inawasaidia kufikia malengo katika kazi na kuboresha utoaji huduma kwa wateja wao pia.

“Benki ya Standard Chartered imeamua kuwa na siku kama hii muhimu kwa ajili ya michezo ambapo wafanyakazi na familia zao wanajumuika pamoja katika michezo mabalimbali, hii inawasaidia kujiweka vyema hata wakiwa kazini,” alisema.

Wakati wa michezo hiyo, washiriki walijumuika pamoja katika michezo mbalimbali ambayo ni pamoja na mpira wa pete, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, kukimbiza kuu, riadha, kuogelea, kucheza muziki na michezo mingine mingi.

Familia ambayo iliibuka mshindi katika mchezo wa kukimbiza kuku iliweza kuondoka na kuku watatu kwa mpigo, wakati zawadi nyingine kama vikombe na nishani zilitolewa katika michezo iliyosalia.

No comments:

Post a Comment