26 July 2012
Wana Tanga waandaa mkutano Dar kujadili mambo mbalimbali
Na Mwandishi Wetu
WAKAZI wa Dar es Salaam waliozaliwa mkoani Tanga, wanatarajia kukutana wiki ijayo kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Mkoa huo likiwemo suala la kushuka kwa maendeleo ya sekta mbalimbali hivyo kukwamisha maendeleo.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Wananchi wa Mkoa huo, Bw. Abdraham Lukindo, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona Mkoa huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Alisema hiyo ni fursa ya pekee kwa wakazi wa Mkoa huo ambao wanaishi jijini Dar es Salaam, kukutana pamoja na kujadili changamoto zilizopo ili kuchochea maendeleo ya kielimu, kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa, kamati hiyo imeandaa mkutano wa pamoja wiki ijayo ambao utaibua mbinu na maarifa mapya ili kuuwezesha Mkoa huo na watu wake kujikomboa katika lindi la umaskini.
Aliwataja baadhi ya watu wanaotarajia kushiriki mkutano huo kuwa ni pamoja na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Yusuf Makamba, mwanasiasa mkongwe Bw. Bakari Mwapachu na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza.
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Joel Bendera na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Bumbuli, Bw. William Shelukindo.
“Imani yetu ni kwamba kikao hiki kitakuwa na mafanikio makubwa kutokana na mawazo ambayo tutayapata kwa wenzetu, tunataka kuona bandari yetu inafanya kazi ipasavyo na kuingiza kipato cha uhakika ambacho kitainua uchumi wa Mkoa na watu wake,” alisema.
Bw. Lukindo aliongeza kuwa, wiki iliyopita walifanya mkutano na wabunge wa Mkoa huo ulifanyika mjini Dodoma ambao ulikuwa na mafanikio makubwa kutokana na michango iliyotolewa.
Alisema wabunge hao waliipongeza kamati yao kwa uamuzi mzuri waliochukua ili kuharakisha maendeleo ya Mkoa huo kiuchumi na kijamii ili jamii kubwa iweze kujikomboa.
“Katika moja ya mambo tuliyokubaliana ni kwenda Mombasa nchini Kenya kuangalia jinsi wenzetu wanavyotoa huduma za bandari na kubaini sababu zilizochangia mizigo ipitie huko,” alisema.
Bw. Lukindo alisema baada ya kurudi huko, wataandaa taarifa ambayo wataomba kumkabidhi Rais Jakaya Kikwete ili iweze kuokoa bandari zilizopo nchini ambazo kwa muda mrefu zimekuwa na sifa ya kuhudumia misigo ya nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia (DRC), Rwanda, Burundi na Uganda.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment