27 July 2012

Wakulima Kondoa wapewa matrekta na diwani wao



Na Darlin Said

WAKULIMA wa Kata ya Kwadelo, Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, wamekabidhiwa matrekta manne yenye thamani ya sh. millioni 80 kutoka kwa Diwani wa kata hiyo, Alhaji Omari Kariati.

Makabidhiano hayo yalifanyika Dar es Salaam jana, katika ofisi za Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT), ikiwa ni mkakati wa kuendeleza sera ya Kilimo Kwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bw. Kariati alisema kuwa, upatikanaji wa matrekta hayo ni utekelezaji wa mpango wa Rais Jakaya Kikwete wa Kilimo Kwanza ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Alitoa wito kwa wakulima kutumia matrekta kama huduma badala ya biashara ili kuwasaidia watu wanyonge kuyatumia kwa bei nafuu ili waweze kutambua msaada wa rais wao.

“Matrekta yatumike kama huduma badala ya biashara ili wanyonge wapate fursa ya kuyatumia ambapo kwa kufanya hivyo, itasaidia kutimiza lengo la rais kuwasaidia wakulima waachane na kilimo cha mkono ili kuongeza uzalishaji mazao,” alisema.

Sambamba na hilo Bw. Kariati alisema kama matrekta hayo yatatumika kinyume na utaratibu waliokubaliana, atalazimika kuyarudisha SUMA-JKT.

Mmoja wa wakulima hao Bw. Halifa Salim, alisema kupitia sera ya Kilimo Kwanza wameweza kulima hekari 100 kwa mwaka wakitumia matrekta tofauti.

“Kipindi cha nyuma nilikuwa nikilima hekari mbili kwa mwaka kwa kutumia jembe la mkono, nawaomba wananchi tushirikiane ili kuondokana na kilimo cha mkono.

Kupatikana kwa matreka hayo, kunafanya idadi ya matreka 20 yenye thamani ya sh. millioni 400 ambayo wamepatiwa wakulima.

No comments:

Post a Comment