27 July 2012

Iundwe mamlaka ya usimamizi vyombo vya majini -Mwaibula


Na Rose Itono

WITO umetolewa kwa Serikali kuunda mamlaka maalumu ya kusimamia masuala yote yanayohusu vyombo vya majini ili kupunguza tatizo la majanga yanayotokea mara kwa mara na kupoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa.

Mdau wa sekta ya usafiri Bw. David Mwaibula aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati mada inayosema “Watanzania tumekubali kuwa Taifa la majanga”, katika kipindi cha Five Connection kinachorushwa na televisheni ya EATV.


Alisema kukosekana kwa Mamlaka hiyo ndio chanzo kikubwa cha matatizo kwa usafiri majini ambapo uwepo wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), hautoshelezi kusimamia masuala ya ajali majini kutokana na kuzidiwa kazi.

Aliongeza kuwa, SUMATRA imekuwa na majukumu mengi kiasi cha kushindwa kusimamia vyema kazi zake hivyo kusababisha matatizo yaendelee kutokea siku hadi siku.

Alisema Serikali ione umuhimu wa kuanzisha mamlaka hiyo ili  kupunguza utamaduni wa kuunda tume ambazo hazina majibu sahihi pale yanapotokea majanga.

“Ni vyema Serikali ikaanzisha Mamlaka ya Majini ili kusimamia masuala mbalimbali kwa umakini na kupunguza ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikitokea majini,” alisema.

Bw. Mwaibula alisema, kumekuwa na ajali zaidi ya mbili lakini kwa sababu SUMATRA imezidiwa kazi, ajali hizo zimekuwa zikiendelea na kupoteza maisha ya Watanzania wengi.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano pale wanapoona vyombo vya usafiri vinakiuka taratibu za usafiri pamoja na kujaza abiria kupita kiasi ili kulinda usalama wao.

No comments:

Post a Comment