09 July 2012

Wajumbe CCM waiunga mkono hotuba ya JK



Na Peter Ringi, Manyara

WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha mapinduzi (CCM), mkoani Manyara, wameiunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyosoma Julai mosi mwaka huu.

Akisoma tamko la wajumbe hao mwishoni mwa wiki kwa waandishi wa habari, Katibu wa CCM mkoani hapa, Bw. Ndengasso Ndekubali, alisema mgomo wa madaktari haukuwa na sababu za msingi kwani Serikali imetimiza sehemu kubwa ya madai yao.


Alisema mgomo huo umesababisha athari kubwa kwa Watanzania ambao baadhi yao wamepoteza maisha kwa kukosa matibabu bila sababu za msingi kutokana na madaktari kukiuka maadili yao.

Bw. Ndekubali aliongeza kuwa, mgomo uliopita nao ulisababisha vifo na kuwaomba madaktari wote nchini kutambua kazi yao ni wito na inahitaji moyo wa huruma si vinginevyo.

“Tunawapongeza kwa dhati madaktari wote wa Mkoa huu kwa kupuuza mgomo na kuamua kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma muda wote hadi sasa,” alisema.

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa,  Bw. Lukas Ole Mukus, alisema imani yao ni kwamba mgomo huo pamoja na ule unaotarajiwa kufanywa na walimu yote ni batili.

“Migomo hii yote ni batili, sisi wanachama wa CCM mkoani hapa tunalaani kwa nguvu zote na kuinga mkono hotuba ya kiongozi wa nchi Rais Kikwete,” alisema Bw. Mukus.

No comments:

Post a Comment