09 July 2012

Mtoto wa miaka miwili na nusu abakwa


Na Salma Mrisho, Geita

MTOTO mwenye umri wa miaka miwili na nusu (jina tunalo), ambaye anaishi na wazazi wake Kijiji cha Buseresere, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, anadaiwa kubakwa na mjomba wake (jina tunalo), mkazi wa kijiji hicho.

Taarifa za awali zinadai kuwa, tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki, saa tatu usiku baada ya mjomba wake ambaye siku hiyo inadaiwa alilewa pombe, kumkuta mtoto sebureni.

Chanzo chetu cha habari kuliongeza kuwa, mama mlezi wa mtoto huyo (jina tunalo), alikuwa chumbani na wadogo zake ndipo mjombe wake alipata fursa ya kufanya unyama huo.

Anadaiwa kuwa, watai mtoto huyo akifanyiwa tendo hilo alianza kulia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata ndipo mjomba wake alimwachia na kutoka nje.

Akisimulia tukio hilo huku akibubujikwa na machozi, mama mlezi wa mtoto huyo alisema, hakuamini kama kaka yake angeweza kufanya kitendo hicho cha kinyama kwa mtoto wao.

“Mtoto alipokuja chumbani huku akionesha nyeti zake huku akilitaja jina la mjomba, nilipomkagua niliona damu zikitililika miguuni mwake,  nilichukua uamuzi wa kwenda kituo Kidogo cha polisi  Buseresere kutoa taarifa.

“Nilipewa PF3 ili niweze kumpeleka mtoto katika Zahanati ya Buseresere kwa ajili ya matibabu,” alisema.

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Bw. Joram Nyanza, alidhibitisha kumpokea mtoto huyo na kudai alikuwa amechanika katika nyeti zake na kumpati matibabu.

“Baada ya kumfanyia mtoto huyu uchunguzi wa kina, tulibaini hakukuwa na dalili zozote za mbegu za kiume hivyo tulimruhusu kwenda nyumbani,” alisema.

Majira lilipomtafuta Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paul, kwa njia ya simu, aliahidi kulifuatilia tukio hilo na kulitolea maelezo.

No comments:

Post a Comment