09 July 2012

Wahimizwa kuyatunza mazingira yawatunze



Na Severin Blasio, Morogoro

MABADILIKO ya tabia nchi yanahofiwa kuangamiza viumbe hai duniani kote baada ya miaka 30 ijayo endepo hakutakuwa na hatua za makusudi ili kukabiliana nayo mapema.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilivyokusanywa na Muungano wa Mashirika na Asasi zisizo za kiserikali wilayani Mvomero (MOC) kwa ushirikiano na The Foundation for Civil society, umebainisha kuwa asilimia 55 ya watu wanakabiliwa na tatizo la mabadiliko hayo.


Miongoni mwa madhara ambayo yalielezwa yanatokana na hali hiyo ni maradhi mbalimbali yakiwemo ya moyo, saratani na shikizo la damu.

Akitoa taarifa ya mradi wa kuelimisha mapambano dhidi ya mabadiliko hayo, athari zake na uundwaji wa Katiba Mpya jana mjini hapa, Mwenyekiti wa MOC Bw. Gaudensia Mchotika na Mkurugenzi wa shirika hilo Bw. Stan Kalala walishauri viongozi kuzitekeleza vema sheria zinazolinda mazingira na wananchi kuhakikisha wanakuwa askari kwa wanaoharibu mazingira hayo.

Walibanisha kuwa, mbali na mataifa yaliyoendelea kuwa mstari wa mbele kuchafua mazingira hususan hewa upo uwezekano wa kudhibiti kazi hiyo endapo viongozi na wananchi watasimama kidete kukabiliana nayo.

"Uchafuzi wa mazingira unagusa mambo makuu matatu, likiwemo la hewa, maji na ardhi ni vita kubwa inayoyakabili mataifa kwa sasa na wenye uwezo wa kujinusuru na janga hili, ni kwanza wananchi kuboresha pale walipo, lakini nao viongozi lazima wazisimamie vema sheria tunazoweka," alifafanua Bw. Gaudensia

No comments:

Post a Comment