09 July 2012

Spika Makinda usikoche kuwafuatilia wabunge watoro


Na Stella Aron

HIVI karibuni kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusiana na vitendo mbalimbali vinavyofanywa na baadhi ya wabunge bungeni na kuonekana kutojali sheria.

Mbali ya wananchi hao kutoa malalamiko hayo pia kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kilizungumza na waandishi wa habari na kuzungumzia hali hiyo.

LHRC ilieleza kutoridhishwa kwake na uendeshaji wa shughuli za Bunge wakati wa mijadala kikisema kuwa, hatua hiyo imesababisha chombo hicho kupoteza mwelekeo.

Taarifa ya kituo hicho imesema, kumekuwa na mapungufu mengi ya uendeshaji wa chombo hicho chini ya Spika, Naibu wake na wenyeviti ambao wanadaiwa kuonyesha upendeleo wa wazi wazi katika usimamizi wa shughuli za Bunge nchini.

Mwanasheria wa kituo hicho ambaye Bi.Imelda Urio,alisema, baadhi ya wabunge hao wameonyesha udhaifu mkubwa katika mkutano wa bunge unaoendelea.

Alisema inasikitisha kuona kuwa, matumizi ya lugha chafu na za kuudhi kinyume na kanuni zinaendelea kutolewa ndani ya bunge, ambalo linapasa kuwa mahali pa kuheshimika kwa ajili ya kujadili mustakabali wa taifa na pia kuwepo kwa mahudhuria hafifu ya wabunge.

Kutokana na hali hiyo kuonekana kukithiri, Spika Makinda sasa amewataka wabunge kuomba kibali kabla ya kuwa nje ya Bunge huku mawaziri wakitakiwa kupata vibali viwili cha Spika na Waziri Mkuu.

Spika Makinda alisema bungeni kuwa sasa ipo haja ya kufanya upya mapitio kwa wabunge kuhusu kanuni na miongozi kwani baadhi ya wabunge wanapoteza muda wakiomba miongozo au kutoa taarifa kwa Spika na kwamba mambo mengi yanayoombewa miongozo hayana umuhimu.

Alisema kuhusu amri ya kuzuia utoro kwa wabunge, Spika Makinda alisema ni lazima wabunge wote wanapotaka kutoka nje ya Bunge waombe kibali kwake na atakayekwenda kinyume na agizo hilo atachukuliwa hatua.

Kwa upande wa kanuni na miongozo ya Bunge, Spika Makinda alisema Bunge linatafuta fedha ili kufanya mapitio kwa wabunge kwa kuwa wengi wanatumia taratibu hizo vibaya na kupoteza muda.

Nionavyo mimi ni kuwa kwanza Spika Makinda tunamshukuru kwa kuliona hilo kwani wapo baadhi ya wabunge katika kipindi cha bunge huwa hawapo bungeni.

Ni vizuri wabunge ambao mpewa nafasi hizo na wapiga kura wenu mkatulia bungeni na kujadili mijadala yenye kuleta maendeleo na si kwa faida yenu.

Vitendo vya baadhi ya wabunge kushindwa kuhudhuria bungeni bila ya sababu maalumu si jambo zuri kwani wapiga kura wenu wanawategemea katika kuwatatulia kero mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Kwa upande wa baadhi ya wabunge wenye kutoa kauli zenye kuudhi ambazo ni za vijiweni ni bora wakaacha kwani wapiga kura wao wanakasirishwa na vitendo hivyo na hata pia husababisha Bunge kuonekana ni sehemu ya kijiwe.

Hatua ya Spika Makinda kuamua kupitiwa upya mapitio kwa wabunge kuhusu kanuni na miongozo jambo hilo litaweza kusaidia kupunguza malumbano yasiyo na msingi yanayotokea bungeni kutokana na baadhi ya wabunge kutofahamu kanuni na sheria za bunge vizuri.

Utolewaji wa lugha chafu bungeni si picha nzuri kwa wapiga kura wenu kwani pia huweza kukuvunjia sifa ya kuweza kushinda tena katika nafasi hiyo kwa kupoteza kura.

Hivi sasa wapo baadhi ya wananchi huamua kuangalia bunge kwa nia kutaka kukosoa na kuwacheka na si kusikiliza hoja zinazoendelea kutolewa na wabunge.

Imefika wakati sasa wabunge wakazingatia kile walichotumwa na wapiga kura nao na si kutafuta sifa kwa kuvunja sheria za bunge ili aweze kuandikwa katika ukurasa wa kwanza kwenye magazeti

1 comment:

  1. sio suala la utoro tu mimi nashangaa kila nikiangalia television wakati bunge linaendelea hata mjadala utakuwa na umuhimu wabunge wengi utawaona wanpiga soga tu na kubembea kwenye viti. Mimi nalaumu sana stareha za bunge letu kuanzia viti mpaka muundo mzima vinawapa wabunge starehe hawaoni shida kabisa ndo maana mpaka wengine wanpiga usngizi. Angalia mabunge mengine tena ya watu matajiri kama uingereza wabunge wamejipanga kwenye viti kama wamo kwenye treni ya daraja la tatu linalokwenda mpanda au kenya sasa sisis eti maskini lakini starehe utafikiri umo ndani ya ndege. kila mmja ana mic yake uingereza wanatumia moja na kenya na kwingineko

    ReplyDelete