02 July 2012

Wafanyabiashara sita kizimbani kwa wizi



Na Rehema  Mohamed

WAFANYABIASHARA sita wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kula njama na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya dola 46,300.

Wafanyabiashara hao ni Bi.Wintyapa Kijugu (35), Bw.Afred Busumubu (35), Bw.Andrew Mayu (38), Bw.Abas Mkurukuru (38), Bw.Elisafu Adiema (45) na Bw.Elias Masiku(48).


Mbele ya Hakimu Bi.Agustina Mmbando,wakili wa serikali Bi.Secilia Mkonongo alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo Mei mwaka huu.

Katika kosa la kwanza ilidaiwa kuwa kati ya Mei mosi hadi 18 mwaka huu ndani ya jiji la Dar es Salaam watuhumiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la wizi.

Katika kosa la pili,wanadaiwa Mei 18 mwaka huu katika Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (PTA) waliiba kontena namba MSKU 1288643 lenye bidhaa mbalimbali zilizokuwa na thamani ya dola 46,300 mali ya Bw.Kapana Thadei.

Watuhumiwa wote walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamiika.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 12 mwaka huu itakapoletwa kwa ajili ya kutajwa.

Watuhumiwa Bi.Kijigu na Bw.Masiku wapo nje kwa dhamana na waliobaki wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza vigezo vya dhamana ambavyo ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh.milioni moja kila mmoja.

No comments:

Post a Comment