16 July 2012
Wachezaji 100 kushiriki Safari Open
Na Mwali Ibrahim
WACHEZAJI gofu 100, wanatarajia kushiriki katika mashindano ya Wazi ya Safari (Safari Open 2012), yatakayoanza leo katika viwanja gofu vya Lugalo, Dar es Salaam.
Miongoni mwa wachezaji hao ni wa wanaounda timu ya taifa ya mchezo huo ya Wanaume ambao ni Frank Roman, Abbas Adam, Nuru Mollel na Jimmy Mollel ambapo washiriki wote katika mashindano wanatoka katika klabu mbalimbali za hapa nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mweka Hazina wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gelase Rutachubirwa alisema wachezaji hao wanatoka katika klabu za Lugalo, Gymkhana ya Dar es Salaam, Gymkhana ya Arusha, Moshi, TPC na Morogoro.
"Mashindano haya yameandaliwa na TGU na yapo katika kalenda yetu ya mwaka ambapo pia wachezaji gofu wanawake watashiriki katika wachezaji waalikwa lakini pia kutakuwa na wachezaji watoto watakaoshiriki pia, na kwamba mashindano haya yatafikia kilele kesho na washindi kutunukiwa zawadi zao," alisema.
Alisema kutakuwa na zawadi kwa washindi ambapo zipo za aina 15 kulinganana na nafasi watakazo zipendekeza kupewa zawadi ambapo zawadi za wanaume, wanawake na watoto zitakuwa zinatofautiana.
Naye kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Shirika la Ndege la Precision ambao ndio wadhamini wa mashindano hayo, Annette Nkini alisema kwa mwaka huu wamedhamini mashindano hayo kwa sh. 3,000,000 ili kuweza kuyafanikisha.
"Precision Air hatutaishia kuyadhamini mashindano haya tu tutaendelea kuidhamini gofu ili iweze kufika mbali na kuwa inafanikiwa katika mashindano yote wanayoyaandaa," Alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment