02 July 2012

Viongozi wazalendo nguzo ya mendeleo nchini



Na Salim Nyomolelo

WAKATI bajeti ya maendeleo ya mwaka 2012/2013 ikiendelea kujadiliwa nchini imedhihirika kuwa, Katiba ya nchi inampa mamlaka makubwa Rais juu ya maamuzi ya Bunge.

Hali hii inatokana na kuwa Bunge kukataa kupitisha bajeti kwa mujibu wa Ibara ya 90 (2) (b) ambapo Rais atavunja bunge jambo ambalo huwapa hofu wabunge wengi kupiga kura ya ndio hata kama ina makosa.

Inaelezwa kuwa katiba imeweka nguvu kubwa kwa Rais kulivunja bunge linapokataa bajeti wakati huo kanuni zimekataza wabunge kupendekeza mabadiliko katika bajeti iliyowasilishwa.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo Bw. John Mnyika anasema kuwa wabunge hawana uwezo wa kubadilisha bajeti na kama ikikataliwa bunge linavunjwa, katika mazingira haya udhaifu wa kushindwa kutumia nguvu za kikatiba una madhara makubwa kwa nchi na maisha ya wananchi.

Bw. Mnyika anasema kupitishwa kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 pamoja na bajeti ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 bila marekebisho ya msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kukosoa kumedhihirisha kile alichohadharisha awali kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kuhusu ya bajeti na uendeshaji wa nchi.

"Katika mazingira haya, udhaifu na uzembe wa bunge unapandikiza migogoro kati ya wananchi na serikali kutokana ufisadi na masuala ya maendeleo kutopewa kipaumbele cha kutosha zaidi ya matumizi ya kawaida lakini pia inachochea migomo baridi ya watumishi wa umma hususun madaktari, walimu na askari kwa madai ya muda mrefu kutozingatiwa katika bajeti," anasema.

Anasema kuwa udhaifu wa kanuni za kudumu za bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu wa kanuni ya 97 (2) ya kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia mambo ya ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote haruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya serikali.

Anasema, wakati katiba mpya ikisubiriwa ni muhimu marekebisho ya haraka kufanyika katika kanuni za kudumu za bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94 mpaka ya 107 ili kuongeza nguvu za bunge katika kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya sasa.

"Katika muktadha huu, nimeanza kufanya uchambuzi ili kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya baadhi ya  kanuni za bunge," anasema Bw.Mnyika

Anasema kuwa kanuni zilizopo kwa sasa zinaongeza mzigo kwa wabunge kutokana na maamuzi ya kutozingatia matakwa ya kanuni za bunge hasa kanuni ya 94 ambayo inalitaka bunge kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ibara ya 63 (3) (c) ya katiba kwa kukaa kama kamati ya mipango katika mkutano wa mwezi Februari ili kujadili na kushauri mapendezo ya mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata.

Anasema mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 Juni 18 mwaka huu na kupitishwa ndani ya siku moja Juni 22 2012 inachangia kufanya bajeti ya nchi isizingatie kwa ukamilifu mpango wa taifa wa miaka mitano bila kujadiliwa kwa kina.

Bw. Mnyika anasema kuwa anamshukuru Spika wa Bunge Bi.Anna Makinda kukiri bungeni Juni 20 mwaka huu kuwa kulikuwa na udhaifu wa miaka mingi wa kutozingatia kanuni ya 106 ambayo inalitaka bunge kujadili muswada wa sheria ya fedha mwishoni baada ya bunge kukamilisha kazi ya kupitisha muswada wa fedha za matumizi ili kuiwezesha serikali kuongeza vyanzo vya mapato kama wabunge walivyopendekeza mwaka jana.

Anasema, izingatiwe kuwa iwapo sheria ya fedha ingepitishwa Juni 22 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali athari zake zingekuwa kubwa kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kwa mujibu wa ibara ya 99 (1) kwa kuweka masharti kwamba bunge halitashughulikia sehemu kubwa ya masuala ya fedha isipokuwa kama amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na bunge.

Anasema kuwa michango na mapendekezo ya wabunge bila Rais kupendekeza isingeliwezesha bunge kufanya mabadiliko ya kupanua wigo wa mapato kwa mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i) ambapo udhaifu ni pamoja na kukatazwa kutoza au kuongeza kodi.

Anasema kamati ya Fedha na Uchumi itumie vizuri ibara ya 99 (3) kurejea maoni yake ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na michango ya wabunge ya mkutano wanne wa Bunge la mwaka jana pamoja na Mkutano wa nane mwaka huu na kufanya marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha kwa kumshauri waziri.

Anasema, ili kuondoa udhaifu uliopo viongozi wanatakiwa kusoma kumbukumbu za bunge (Hansard) za Juni 18 hadi 22 mwaka huu na kuliongoza baraza la mawaziri kumwezesha waziri wa fedha kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au mabadiliko yanayopaswa kufanyika ili kupunguza kodi katika bidhaa kuchangia mfumuko wa bei na kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi kwenye vyanzo mbadala vilivyoelezwa bungeni.

"Nawashukuru pia viongozi wa dini, chama na asasi mbalimbali nje na ndani ya serikali walionipa moyo wa kuendelea kusimamia ukweli na kuacha unafiki ili kusimamia uwajibikaji wa viongozi kwa maendeleo ya taifa," anasema Bw.Mnyika

Anasema, ataendelea kuamini kuwa kutamka neno udhaifu wa Rais sio kumtukana Rais na wala sio kulitumia jina lake kwa dhihaka ila pamekuwepo na mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi hadi kutolewa nje ya ukumbi wa bunge.

Anasema anakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha kumbukumbu sahihi kuwekwa.

Anasema kuwa Katiba ya nchi walioapishiwa kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba, sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndio chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri serikali.

"Tangu nichaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010 kwa nyakati na maeneo mbalimbali viongozi wa vyama, dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusu viongozi wakuu kutumia nguvu na mamlaka ya kikatiba kuiongoza kwa uthabiti serikali kushughulikia masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayolikabili taifa," anasema Bw. Mnyika

Anasema kuwa Juni 19 mwaka huu alieleza bungeni kabla ya kutolewa sababu za kuikataa bajeti kwa kutokuweka misingi thabiti ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei.

Anasema kuwa kiwango cha fedha kwa ajili ya miradi ya barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam ikiwemo jimbo la Ubungo ni kidogo tofauti na kile kilichotajwa na kuingizwa katika jedwali la Mpango wa Taifa wa miaka mitano kwa upande wa miradi ya maendeleo iliyopaswa kutengewa fedha katika bajeti ya 2012/2013.

"Tuliamua kuikataa bajeti kwa kuwa ilishindwa kuzingatia mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano ambao uliowasilishwa na kupitishwa kwa azimio la bunge ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo kama zilivyokokotolewa katika mpango husika," anasema Bw. Mnyika

Anasema kuwa anaamini kuwa Rais Kikwete ana nafasi ya kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza nguvu zake katika muswada wa sheria ya fedha kupanua wigo wa mapato.

Anasema kwa upande wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam, serikali inapaswa kuwasilishwa nyongeza ya fedha za miradi ya maji kwa upande wa Ruvu juu pamoja na ujenzi wa Bwawa la Kidunda.

Anasema serikali iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami barabara za pembezoni za mchujo na za mzunguko ili kupunguza msongamano wa magari.

Anasema kuwa baadhi ya makosa husababishwa na  woga ambapo kiongozi anashindwa kumlaumu mkubwa wake hata kama kuna makosa ameyafanya na kuongeza kuwa msingi wa woga ni ubinafsi.

"Woga wa ubinafsi huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha ili wasije wakatuchukia," anasema Bw. Mnyika


1 comment:

  1. MABUNGE YOTE CHINI YA JUMUIYA YA MADOLA MIFUMO YAKE YA KUENDESHA VIKAO VYA BUNGE TATIZO NI KUCHAKACHUA KUTOKANA NA WENGINE KAMA TANZANIA KUTUMIA SIASA YA UJAMAA WAKATI UINGEREZA NI UBEPARI ,UINGEREZA KUNA MABUNGE MATATU "HOUSE OF LORDS,HOUSE OF SENATES NA HOUSE OF COMMONS" BUNGE LA TANZANIA LINATAKA LIJIPATIE MADARAKA YA JUU LIKIJIONA LIKO JUU YA MABUNGE YOTE KWANGU HILI KATIKA MFUMO WA UBEPARI NI 'HOUSE OF COMMON:SINA UHAKIKA NDILO LENYE MADARAKA YA MWISHO HUKO UINGEREZA NI UKOSEFU WA UELEWA WABUNGE WA CHAMA TAWALA KUPINGA BUDGET YAO WALIYOKUBALIANA KWENYE PARTY CAUCAS BUNGE LILILOENDESHWA NA SAMWEL SITTA NDIPO VURUGU ZILIPOANZIA WAPO WALIOFURAHIA MAPUNGUFU HAYO HUSUSAN WAPINZANI

    ReplyDelete