27 July 2012
Uzalendo unahitajika kusimamia uchimbaji gesi- Killagane
Na Cornel Antony
MATUMIZI mabaya ya rasilimali ni moja ya kikwazo cha maendeleo katika nchi zinazoendelea.
Licha ya kuwa kipimo cha utajili wa Taifa ambao husaidia kuongeza fedha za kigeni, usimamizi wake umekuwa ukisuasua huku wachache wakinufaika nazo.
Zipo rasilimali za asili na zile zilizotengenezwa na binadamu. Maliasili hai na zisizo hai, zikijumuisha watu, wanyama na mimea wakati zile zisizo hai ni kama madini ya ardhi.
Huo ni utajiri kwa upande wake mmoja lakini kiuchumi rasilimali isiyotumika ni utajiri usiokuwa na thamani, kwa hivyo basi ili ziwe na thamani na manufaa kwa binadamu lazima zitumike.
Changamoto iliyopo ni jinsi gani ya kutumia rasilimali hizi kiuendelevu, ili kuzilinda hususan zinazoweza kuzalishwa kama vile madini, gesi ya asili na mafuta.
Tunatakiwa kuzitumia kulingana na juhudi zetu za uzalishaji ili kuhakikisha kuwa zinadumu na kuleta tija kwa manufaa ya kizazi cha leo na cha kesho.
Ukweli ni kuwa ili kuzisimamia rasilimali za asili ziwe endelevu lazima kuwa na uzalendo, ili kujenga mfumo utakaomwajibisha kila mmoja wetu atakaepewa jukumu la kuongoza jahazi hilo.
Moja ya mashirika yanayolinda rasilimali hizo ni Shirika la Maendeleo la Petrolium Tanzania (TPDC), lilioanzishwa chini ya sheria ya Mashirika ya Umma namba 17 ya mwaka 1969 kwa agizo la Rais Government Notes namba 140 mwaka huo.
Chini ya sheria TPDC ilianza kazi mwaka 1973 na mwaka 1980 ilipishwa sheria ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta ya mwaka 1980 Petrilium Exploration and production Act (1980).
Mafanikio yake ni pamoja na kuvutia makampuni ya kimataifa kuja kuwekeza katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia na ugunduzi wake maeneo ya Mkolonga, Songosongo Kusini, Kiliwani Note, Ntobya na Mnazi bay Mtwara.
Shirika hilo limeonesha nia njia ya kuwa jukumu walilokabidhiwa limeanza kuzaa matunda Mikoa ya Mtwara na Lindi kwani Watanzania wameanza kuonja matunda lakini sasa shirika hili limekuja na nguvu mpya kuinua uchumi wa Taifa.
Hivi karibuni ilikakikabidhi ujenzi wa bomba la mradi wa gesi Mkoani Mtwara utakao jengwa na kampuni tatu za kutoka nchini China kutoka Mtwara hadi Somanga Dar es-salaam.
Mradi huu ukikamilika utaokoa fedha nyingi kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kuzalisha umeme na kupunguza tatizo la mgao linaloikabili nchi.
Usimamizi thabiti wa Mkurungenzi mtendaji wa TPDC Bw. Jona Killagane umesaidia kwa kiasi kikubwa kulindwa rasilimali hiyo.
Bw. Killagane anasema TPDC ni moja ya kati ya mashirika inayosimamia rasilimali ya gesi ya asili na mafuta nchini kutokana na umuhimu wake katika kuinua uchumi.
"Naomba wana Mtwara na Watanzania wote watamue kwamba bomba la gesi litakalo toka Mtwara kwenda Dar-es-salaam ni hazina ya kila mmoja wetu, nimefarijika sana kuwaona wana Mtwara na Songosongo mkoani Lindi kuunga mkono miradi hii kwa kuweza kuwapa ushirikiano wataalam mbalimbali waliofanikisha," anasema
Anasema uchimbaji wa gesi bila kubugudhiwa na wananchi ni ishara ya kuwa wameona umuhimi katika maendeleo yao na taifa.
"Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi kupitia kwa mkuu wa mkoa kwani wananchi wengi wasipoandaliwa kupokea mradi wanaweza kugoma kutoa ushirikiano," anasema Bw.Kallagane.
Anasema baadhi ya malengo yaliyowekwa yamefikiwa na ikiwemo utafutaji wa gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini.
"Naamini baada ya miaka michache Tanzania itakuwa moja ya nchi zitakaozalisha uwingi wa gesi duniani," anasema.
Serikali imeamua kujenga na kumiliki bomba kuu litakalo unganisha rasilimali za gesi za Mnazi Bay, Ntovya Songosongo, Kiliwami, Nyumi, Mkua na Gesi iliyogunduliwa kwenye kina kirefu cha maji.
Anasema mradi huu utakapokamilika utawezesha upatikanaji wa gesiasilia kiasi cha 784 mmstd ifikapo mwaka 2020, ili kupunguza zaidi ya dola za Marekani bilioni 1 kwa mwaka kwa kutumia mafuta badala ya gesi asilia.
Bw. Killagane ameahidi kuzipa kipaumbele changamoto nyingi kwenye shirika hilo lakini peke yake hawezi kuzitatua anahitaji kuungwa mkono ila mtu kwa nafasi yake kuanzia kwenye kaya hadi Taifa hata kwa mwananchi mmoja.
Serikali pia imetengeneza zaidi ya dola 114 milioni za Marekani kutokana na mauzo ya gesi tangu wakati huo. Miradi ya gesi nchini imesaidia pia kupunguza hewa chafu itokanayo na matumizi ya mafuta katika mitambo.
Tumsaidie bw. Killagane kwa kuongoza sekta hii muhimu iliyobeba uchumi wa Taifa lenye changamoto nyingi zinazokwamisha maendeleo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment