27 July 2012

Simba kufanya usajili upya



Na Elizabeth Mayemba

BAADA ya timu ya Simba kuondolewa katika michuano ya Kombe la Kagame na Azam FC hatua ya robo fainali, uongozi wa klabu hiyo umepanga kuongeza wachezaji wengine katika kikosi hicho.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa viongozi wa Simba ambaye yumo katika Kamati ya Usajili, alisema timu ina upungufu katika nafasi ya beki wa kulia, kushoto na wa kati kwa kuwa waliopo sasa nafasi ya kati aina yao ya uchezaji unafanana.


"Timu yetu si mbaya sana lakini kuna kasoro katika safu ya ulinzi na ushambuliaji, hivyo tunatakiwa kufanyia marekebisho haraka kabla ya usajili kufungwa," alisema kiongozi huyo.

Alisema pia kukosekana kwa mabeki wa kushoto Amir Maftah na Said Nassoro 'Chollo' wa kulia ambao ni majeruhi, pia kumechangia kwa kiasi kikubwa timu kuboronga, ndiyo maana wataongeza mabeki wengine katika safu hiyo ili ikitokea mmojawapo akiumia pengo lake linazibwa.

Kiongozi huyo alisema pia ushambuliaji katika kikosi hicho bado ni tatizo na pengo la mshambuliaji Emmanuel Okwi bado linaonekana, ingawa mshambuliaji mpya Abdallah Juma anaonekana kumudu vyema akishirikiana na wenzake, lakini wanahitaji kuongeza mwingine.

Okwi anaendelea na majaribio katika klabu ya FC Red Bull Salzburg ya Austria na majibu yake yanatarajiwa kutolewa wiki ijayo endapo atakuwa amefuzu au la.

Alisema safu ya kiungo imeenea, hivyo katika marekebisho ya usajili safu hiyo hawataigusa kwa kuwa imejitosheleza na hakuna pengo kubwa ila kocha bado anakazi ya kuirekebisha vizuri zaidi.

Baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Kagame wachezaji wote wa Simba, wamepewa mapumziko ya wiki moja na kocha Milovan Cirkovick ambaye anakwenda kwao Serbia kwa mapumziko mafupi na atarejea wiki ijayo kwa ajili ya programu zake za mazoezi.

No comments:

Post a Comment