27 July 2012
Uhaba wa vifaa wachangia taka kuzagaa Dar
Na Rehema Maigala
TATIZO la uhaba wa vifaa vya kuzolea taka katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam, unachangia jiji hilo kuwa chafu.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, katika warsha ya kupata mawazo ya wadau mbalimbali wa mazingira ili kuwezesha jiji hilo kuwa safi, Kaimu Mkuu wa Udhibiti Taka mkoani humo, Bw. Protus Membe, alisema jiji hilo lina uhaba wa vifaa vya kuzolea taka kwa asilimia 94, pamoja na magari 42 ya kuminya taka.
Alisema taka ngumu kama zilizopo hospitali, wanashindwa kuziteketeza kwa sababu ya ukosefu vifaa na hazifai kutengeneza mbolea ambayo inahitajika.
“Ndio maana tumeshirikisha wadau kutoka sehemu mbalimbali vikiwemo vikundi vya kijamii ili kupata mawazo yao na kuliweka jiji letu katika hali ya usafi,” alisema Bw. Membe.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Didas Masaburi, hivi sasa jiji hilo linakadiriwa kuzalisha wastani wa tani 4,252 za taka kwa siku ambazo kati ya hizo, asilimia 26-37 ni taka ambazo zinatupwa dampo.
Alisema Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na taasisi za Scinap na Borda, wameanzisha sehemu ya kutengeneze mbolea ya mboji kwa kutumia taka rejea ambazo ni mabaki ya vyakula mbalimbali kutoka katika Kata ya Buguruni Kisiwani kwa kushirikiana na Kikundi cha Mazingira cha Kisiwani (KEG).
Dkt. Masaburi alisema taka rejea na mbolea ya mboji ni vyanzo vya mapato kwa vikundi vya kijamii vinavyojihusisha na udhibiti wa taka jijini hivyo kupata kipato kupitia taka hizo.
“Mbolea ya mboji inahitajika kwa kiwango kikubwa na wakulima wadogo jijini Dar es Salaam ambao wanalima kilimo cha mbogamboga na matunda hivyo kuna baadhi ya taka ambazo zinafaida kwa jamii,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment