Na Mwandishi Wetu, Longido
VIJANA wa Kimasai (Morani) zaidi ya 500 kwenye kata ya Engerenaibor, iliyopo Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, wanadaiwa kumuua Meneja wa Mgodi wa Madini aina ya Ruby, uliopo Mundarara Ruby Mining Company Ltd, Bw. Omary Shengovi (49), kwa kumchoma moto.
Bw. Shengovi alikuwa amelala katika nyumba ya kampuni hiyo ambayo morani hao waliivamia na kuichoma moto akiwa ndani.
Katika tukio hilo la kinyama, Bw. Shengovi alikutwa na mauti akiwa bafuni ambako alikwenda kujificha ili kujihami na morani ambao pia waliichoma moto gari ya kampuni hiyo aina ya Toyota Pick-up Double Cabin, yenye namba za usajili T 885 AMN.
Gari nyingine iliyoteketezwa kwa moto ni lori aina ya Scania yenye namba za usajili T 798 AXB, mashine za upepo migodini ambazo zilichomwa moto na kuharibika pamoja na kufanya uharibifu wa mali zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 300.
Morani hao wanadaiwa kutumia mafuta ya petroli katika kufanya unyama huo wakati watumishi wengine wa mgodi huo zaidi ya 65 wakiwa wamekimbia vichakani wakihofia maisha yao.
Baada ya kufanikisha azma hiyo, morani hao walitokomea kusikojulikana ambapo ilipofika alfajiri, watumishi wa mgodi huo walianza kutafutana morani hao na kugundua Meneja wao ameuawa.
Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio zinadai kuwa, saa moja kabla tukio hilo, kuna watu ambao walivunja uzio wa mgodi huo upande wa Magharibi na kuingia mgodini.
Wakiwa ndani ya mgodi, walianza mapambano na skari ambapo mmoja kati ya watu hao (jina tunalo), alipigwa risasi ambapo wenzake walimbeba na kuondoka naye lakini alikufa muda mfupi akiwa nje ya uzio.
Kutokana na hali hiyo, morani walipiga yowe usiku huo, kukusanyika na kuvamia mgodi huo ili kulipa kisasi wakidai mtu wao ameuawa nje ya uzio wa mgodi huo.
Akizungumza na Majira, Mdhibiti Mkuu wa Madini mgodini hapo, Bw. Mohamed Shakihiyo, alisema tukio la uvunjaji uzio wa mgodi lilitokea kati ya saa nne na tano usiku.
“Ghafla tuliona kundi kubwa la vijana limevunja uzio na kuingia ndani na kuwasaka watumishi nyumba hadi nyumba, walipofika katika nyumba ya Bw. Shengovi, waliiwasha moto, kuendelea kufanya uharibifu wa mali zingine.
Kutokana na hali hiyo, timu tatu za Serikali kutoka Ofisi ya Madini Kanda ya Kaskazini, Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani Arusha na Wilaya ya Longido, Ofisa Taarafa ya Longido, Bw. Peter Kakanyi ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo la hilo, Bw. Lekule Laizer, walikagua mgodi huo na kukutana kwa dharura na uongozi wa kampuni hiyo.
Kampuni hiyo inaongozwa na Mkurugenzi wake, Bw. Philip Mkenga 'Jungle Master', ambapo pamoja na mambo mengine, uongozi huo, Serikali na mila za kabila hilo, walieleza kusikitishwa kwao na tukio hilo wakidai ni maara ya kwanza kutokea.
“Kimsingi kuna mahusiano mazuri kati ya wamiliki wa mgodi na majirani, sijui kimetokea nini katiika tukio hili ambalo limetuuma sana,” alisema Ofisa Tarafa ya Longido Bw. Kakanyi na kuongeza kuwa, wanawake wamegoma kula wakilaani kitendo hicho.
Mbunge wa jimbo hilo, Bw. Laizer alisema maeneo yote ya madini duniani yana migogoro lakini kwa Mundarara kuna unafuu mkubwa kwani watumishi wanashirikiana sana na wananchi.
“Tunawahakikishia tukio kama hili halitatoke tena, tunaomba mtuamini sisi mbali na nyadhifa zetu serikalini, viongozi wa kimila mbali na kukutana leo (juzi), tutakuwa na mkutano tena kesho (jana) na wananchi ambapo Mkuu wa Wilaya atakuwepo,” alisema Bw. Laizer.
Jeshi la Polisi lilidai uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ambapo hivi sasa wanamshikilia askari wa kampuni hiyo Bw. Abeli Shauri kwa uchunguzi zaidi.
Licha ya watumishi wa mgodi huo kuhakikishiwa usalana wao, bado waligoma kuendelea kuishi eneo hilo ambapo Mkurugenzi wao Bw. Mkenga alilazimika kutumia nguvu ya ushawishi na kuliomba Jeshi la Polisi kuendelea kufanya doria katika eneo hilo hadi watumishi hao watakaporidhika kuwa amani imerudi.
Mwili wa Bw. Shengovi ulichukuliwa na polisi na kupelekwa Hospitali ya Longido ili kufanyiwa uchunguzi na baadae ulikwenda kuhifadhiwa kwenye mochali ya Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru ambapo jana ulitarajiwa kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Soni-Lushoto, mkoani Tanga kwa mazishi.
No comments:
Post a Comment