26 July 2012
Uchimbaji madini unufaishe wazawa
HIVI karibuni, washiriki wa mkutano wa 16 uliohusisha wataalamu wa masuala ya uchumi na madini, walijadili kwa kina umuhimu wa sekta hiyo kunufaisha wazawa.
Mkutano huo ambao ni wa kwanza kufanyika nchini, uliandaliwa na Umoja wa Umoja wa Mataifa (UN), ili kupitia kanuni za uchimbaji madini yasitumike kibiashara pekee na kusafirishwa nje ya nchi bali yanufaishe wananchi.
Katika mkutano huo, Mwakilishi wa UN katika Tume ya Uchumi ya Afrika inayoshughulikia Miundombinu na Maendeleo ya Maliasili, Bw. Soteri Gatera, alisema pamoja na nchi nyingi barani Afrika kuchimba madini siku hadi siku, hakuna kizazi kilichonufaika na rasilimali hiyo hadi sasa.
Alisema wananchi walio katika kundi maskini ndio hawanufaiki kabisa na uchimbaji huo ili waweze kujikomboa katika lindi la umaskini, kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Sisi tunasema kuwa, Tanzania ina migodi mingi mikubwa ambayo kama Serikali itahakikisha inatumika kikamilifu ili kunufaisha wananchi, umaskini uliopo nchini utapungua kwa kiasi kikubwa hasa kwa Watanzania waishio vijijini.
Upo umuhimu mkubwa wa madini na rasilimali nyingine, kunufaisha wazawa wa makundi yote badala ya kikundi cha watu wachache.
Imani yetu ni kwamba, Mungu aliumba dunia na kuwapa watu haki sawa katika kuitawala hivyo kila mtu ana haki ya kunufaika na rasilimali zilizoko duniani.
Kitendo cha nchi tajiri kutumia uwezo wa kiteknolojia kuchukua madini yaliyopo katika nchi maskini kama Tanzania ni udhalilishaji mkubwa na hatari kwa ustawi wa nchi husika.
Ipo haja ya kufanya mazungumzo ya kina kuhusu matumizi ya rasilimali za dunia kati ya nchi tajiri na maskini ili kuweka uwiano sawa wa faida ya rasilimali zilizoko duniani na kuondoa unyonyaji.
Kitendo cha nchi tajiri kutumia fursa ya umaskini wa nchi maskini na kuwekeza ili kujilimbikizia mali, kinapaswa kujadiliwa upya na kutoa fursa sawa ya mgawanyo wa rasilimali.
Ukweli ni kwamba, nchi maskini zinakubali kutoa rasimali zao kwa nchi tajiri kutokana na kukosa uwezo wa kuziendeleza jambo ambalo nchi tajiri inatakiwa kuliangalia na kuziwezesha nchi maskini ili ziweze kunufaika na rasilimali zake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment