26 July 2012

Ukataji tiketi kwa njia ya simu utapunguza ulanguzi kwa abiria


Na Salim Nyomolelo

MAENDELEO ya Teknolojia yamerahisisha huduma za jamii ikiwemo mawasiliano ya simu yanayounganisha watu sehemu mbalimbali nchini.

Awali mawasiliano yalitumia barua ambayo ilichukua muda mrefu kumfikia mlengwa na kupata mrejesho.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kiasi kikubwa yamesaidia katika sekta ya elimu, afya na kazi za kila siku ambapo matumizi ya komputa yamerahisisha kazi.

Huduma huwafikia wananchi kwa urahisi kutokana na utandawazi pamoja na uboreshwaji wa huduma unaofanywa kwa njia ya simu za mkononi.

Matumizi ya simu za mkononi yamesaidia kupunguza gharama kwa watumiaji kwa kuepuka gharama za kusafiri umbali mrefu ili kuweza kupata huduma mbalimbali.

Kabla ya teknolojia hii wananchi walikuwa wanakaa kwa muda mrefu kupokea huduma kwa maana pesa, vifurushi mbalimbali na barua jambo ambalo lilisababisha kupokea taarifa kwa kuchelewa.

Teknolojia ya simu imeweza kuendelea siku hadi siku na kurahisisha utoaji wa huduma kwa walengwa ambapo kwa sasa wananchi wanaweza kupata huduma ya tiketi mbalimbali za safari kupitia simu zao za mkononi bila kufika katika ofisi ama kituo cha mabasi ya mikoani na nje ya nchi.

Mkurugenzi wa biashara na maendeleo wa kampuni ya mobile ticketing limited kwa kushirikiana Selcom paypoint Bw.Costa Mtungwa anasema kuwa tayari wamezindua huduma mpya na rahisi ya kukata tiketi za mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani kupitia mashine za Selcom Paypoint.

Anasema huduma hiyo inajulikana kama tiketi popote na pay point ambayo ni ya kipekee na ya kwanza Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla ambayo inamsaidia mwananchi kuepukana na gharama pamoja na usumbufu wa kutembea kwa muda mrefu kupata huduma.

Anasema kuwa inamsaidia mtu kutopoteza muda wa kutembea umbali mrefu na badala yake muda huo atautumia kwa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo yake.

Bw. Mtungwa anasema kuwa baada ya kufanikiwa na huduma hiyo kwa kushirikiana na Kampuni ya Mawasiliano ya vodacom, abiria wanakata wanapata fursa ya kukata tiketi  za mabasi kwa kutumia simu ya mkononi.

"Tumechukua fursa ya kuanzisha huduma hii baada ya kutambua uwepo wa kundi la watu ambao wanapata usumbufu wa kutembea umbali mrefu pamoja na kupoteza muda mwingi ili kuweza kupata huduma ya tiketi," anasema Bw. Mtungwa

Bw. Mtungwa anasema kuwa huduma hiyo inalenga kuboresha utaratibu wa kukata tiketi kwa kutumia simu ya mkononi pamoja na kuendelea na kuondoa utaratibu ambao umepitwa na wakati ambao una usumbufu mkubwa kwa abiria.

Anasema kuwa badala ya abiria kufika kwenye ofisi za basi husika ili kukata tiketi anatumia simu yake ya mkononi jambo ambalo litamsaidia kuepukana na tatizo la  kuzidishiwa nauli linalo fanywa na madalali.

Anasema kuwa wakati wa msimu wa sikukuu abiria hupata usumbufu hasa katika kuuziwa tiketi moja zaidi ya watu wawili jambo ambalo huleta usumbufu usio wa lazima kwa abiria na hata mara nyingine usababisha ucheleweshwaji wa kuanza kwa safari kwa kufanya jitihada za kutatua tatizo la namna hiyo.

Anasema kuwa ili kuweza kupata huduma hiyo abiria anatakiwa kutembelea kituo cha Selcom Paypoint na kutoa taarifa ya safari yake ambapo ataingiza taarifa  zake ikiwamo na aina ya basi analohitaji, tarehe ya kusafiri pamoja na mahala anaposhukia ambapo tiketi itakuwa printed.

Anasema kuwa huduma hiyo inapatikana katika vituo zaidi ya 600 katika mkoa wa Dar es Salaam pamoja na maduka ya kawaida, maduka ya mkulima, stationeries, supermarkets na kwa mawakala wa huduma za kifedha za simu za mkononi M- Pesa na Airtel Money.

"Abiria atatutumia tiketi hiyo kumtambulisha na kwa ajili ya kupanda basi siku ya safari yake bila ya usumbufu wa aina yoyote na atakuwa ameepukana na usumbufu kama ilivyokuwa awali," anasema Bw. Mtungwa.

Anasema kuwa hadi kufikia sasa kampuni za mabasi kumi  tayari zimeweza kuboresha huduma zao kwa kujiunga na huduma hiyo ambapo mabasi hayo yanasafiri mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Singida, Dodoma, Bukoba, Kigoma na nchi za jirani.

Anasema kuwa huduma hiyo kwa sasa inapatikana katika mkoa wa Dar es salaam na mchakato unaendelea ili kuweza kuifikia mikoa yote nchini na vyombo vingine vya usafiri ndani ya muda mfupi ambapo baada ya hapo mkoa wa Mwanza utafikiwa na huduma hiyo.

Bw. Mtungwa anasema kuwa huduma hii itaenea mikoa yote ya Tanzania licha ya wananchi wengi kuzoea kulipia baadhi ya huduma nyinginezo.

Anasema kuwa huduma hiyo haina gharama yoyote ambazo abiria anatozwa ili kufanikisha upatikanaji wa tiketi na atalipa fedha ya nauli halali iliyopendekezwa na serikali.

Anasema kuwa huduma hiyo inampa fursa abiria kutoa taarifa ya kuahirisha safari yake kabla ya masaa sita ya safari kuanza ambapo fedha zitarudishwa kwake kupitia simu ya mkononi bila ya makato yoyote.

Anawataka wadau wote hususani serikali na vyombo vya habari kuhamasisha umma na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya huduma hiyo kwa sababu ina faida ikiwa ni pamoja na kuokoa  muda, nguvu,  fedha, rasilimali nyingine pamoja na  maendeleo kwa Taifa.



No comments:

Post a Comment