06 July 2012

Tuwasaidie yatima, watoto wa mitaani



KITANDA usichokilalia, huwezi kujua kunguni wake ambapo shida na mateso wanayopata watoto waishio katika mazingira hatarishi na wale wa mitaani ni vigumu kuelezea.

Watoto hawa hawajui leo au kesho watakula nini, hakuna anayehangaika kuwatafutia chakula. Wanapolala na njaa hakuna wa kumlilia ambapo wakiumwa hakuna wa kumweleza hivyo huendelea na maisha yao hadi wanapopata nafuu na kupona kabisa.


Ukweli ni kwamba, watoto hawa hujisikia wapweke na waliokataliwa na ndugu zao, Serikali na jamii kwa ujumla.

Jambo la kusikitisha, idadi kubwa ya watoto, umri wao unaanzia miaka mwili hadi 10 ambao kimsingi hawajui kujitegemea, njaa ikiuma wanalia tu na kushindwa kujieleza.

Kitanda chao ni barabarani na wengine mitaroni, baridi yote ya usiku na jua la mchana ni lao, hawajui kubadilisha nguo, zile walizovaa wiki iliyopita hadi leo hazijatoka mwilini.

Tumezoe kuwaona watoto wenye wazazi wakitoka nyumbani asubuhi na kurudi nyumbani kwao jioni. Watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi wanarudi wapi, wakitoka hawajui wanakwenda wapi.

Jamii imesahau kuwa watoto hawa ni sawa na wao, wanasikia njaa, baridi na maumivu sawa na wenzao lakini nani anashughulika nao?

Sisi tunasema kuwa, watoto hawa hawakuchagua kuwa yatima na kuishi mitaani, hawakuchagua kufiwa na wazazi wao, wamejikuta  wapo mitaani na hawana la kufanya kama watoto wetu walivyojikuta wakiwa mikononi mwetu na wanapata kila kitu.

Waswahili wanasema, kinga ni bora kuliko tiba. Mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs na yale ya kimataifa kama UNICEF na Serikali, wanashughulikia tatizo la watoto hawa wakiwa tayari mitaani.

Jambo la msingi, nguvu inayotumika kuwasaidia watoto hawa ingepaswa kuelekezwa kwenye kinga ili kutibu tatizo hilo kabisa. Sababu moja wapo inayochangia ongezeko la yatima na watoto waishio mazingira hatarishi ni migogoro isiyokwisha katika ndoa.

Hatua za haraka zinahitajika ili kupunguza au kumaliza tatizo la watoto wa mitaani na yatima kwa kuwaunganisha na walezi pamoja na ndugu zao ambao tunaamini wapo.

Umefika wakati wa Serikali kuratibu nguvu hizi kwa kuhakikisha mashirika hayo, jamii na wao wenyewe wanachukua hatua stahiki za kuhakikisha tatizo hilo nchini linapata ufumbuzi wa kudumu.


No comments:

Post a Comment