24 July 2012

Tukuyu Stars sasa imeanza kukamilika



Na Janath Abdulrahimu

JUHUDI za kuifufua Tukuyu stars zimeendelea katika kata na tarafa mbalimbali za jiji la Mbeya na mpaka sasa wapo katika hatua ya nusu fainali kwa ajili ya kupata wachezaji wa kuunda timu hiyo.

Akizungumza Dar es salaam jana Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo Peter Mwambuja alisema lengo la kuifufua timu hiyo ni kubadilisha mpira wa Tanzania uwe katika sura ya mpira wa zamani, kwa kuzalisha wachezaji wenye nidhamu na uwezo mkubwa wawapo uwanjani.


Mwambuja alisema matarajio yao si kuwa na wachezaji 30 tu bali watakuwa na wachezaji zaidi ya 200 ambao watawauza katika klabu mbalimbali.

"Hatutarajii kununua wachezaji kutoka nje kuichezea timu yetu, bali tunaanzisha kitalu ambacho kitakuwa kinazalisha wachezaji ambao tutawauza katika klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi  na wengine kuiendeleza timu yetu," aliema Mwambuja.

Fainali za mchakato huo zinatarajiwa kufanyika tarehe Agosti 4, mwaka huu ambapo wachezaji wakongwe wa timu ya Veteran waliopo Mbeya wataumana na wale waliopo Dar es Salaam ili kuleta hamasa kwa wachezaji wapya,
pia siku hiyo kutakuwa na ngoma za asili maarufu kama Mangoma na Ipenenga ikifuatiwa na kongamano ambapo wadau watajadili jinsi ya kuifufua na kuiendeleza timu hiyo.

Makamu mwenyekiti huyo amewataka wadau wenye mapenzi  na timu hiyo kujitokeza kuchangia vifaa,fedha na mawazo yanayoweza kuiendeleza timu hiyo na kusisitiza kuwa kila Ijumaa huwa wanakutana katika ukumbi wa wazee uliopo Ilala, Dar es salaam kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuifufua timu hiyo, ambapo  mazoezi kwa maveterani wao huwa yanafanyika kila Jumamosi Uwanja wa Habours club uliopo Kurasini, Dar es salaam.

Alisema wanatarajia kutumia fursa hiyo kuvitangaza vivutio mbalimbali vilivyopo mkoani humo ikiwa ni pamoja na Daraja la Mungu.

Pia ametoa wito kwa mikoa mingine kufanya kama walivyofanya wadau wa Mbeya, kwani kuna vipaji vingi vipo vijijini lakini vinakosa mwongozo.

No comments:

Post a Comment