24 July 2012
Mbato Cup kuanza kutimua vumbi Agosti
Na Omary Mngindo, Bagamoyo
MICHUANO ya kuwania kombe la Diwani Shukuru Mbato (Mbato Cup) Kata ya Pera Bagamoyo, Pwani inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Diwani Mbato kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Pingo ambapo alisema michuano hiyo itafanyika mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Michuano ya mwaka huu yataongezeka ushindani kutokana na kuongezwa timu kutoka nane na kufikia 12, ambapo kutakuwa na timu waalikwa kutoka kata jirani ambazo zitafahamika hapo baadaye,” alisema Mbato.
Aidha alieleza kwamba kwa sasa wapo katika harakati za kukusanya zawadi kwa washindi ambazo zitakuwa bora zaidi ikilinganishwa na za msimu uliopita, hivyo amewataka viongozi kuendelea na maandalizi kwa timu zao.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wa timu shiriki kuendelea na mawindo ya michuano hiyo, kwani yapo mbioni kuanza ambapo ni mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani,” alisema Diwani huyo.
Wakati huohuo mdau wa michezo ndani ya Kata hiyo Hamis Fedha ameandaa michuano ya kuwania mnyama mbuzi kwa kushirikisha timu saba zilizoko ndani ya Kata hiyo.
Mratibu wa michuano hiyo Fedha alisema michuano hiyo inafikia tamati leo na yameandaliwa kwa ajili ya maandalizi ya kombe la Mbato.
Fainali hiyo inazikutanisha timu za Bogota Fc na Magome Fc ambazo zimetinga hatua hiyo ambapo Bogota iliifunga Bodaboda kwa mabao 3-1 na Magome iliifunga Dubai bao 1-0.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment