26 July 2012
TRA kutoa mafunzo ya ukusanyaji kodi
Na Salim Nyomolelo
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ili waweze kukabiliana na mabadiliko ya ukusanyaji kodi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Harry Kitillya mafunzo hayo yatatolewa kwa ushirikiano wa mamlaka hiyo na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa upeo wafanyakazi ili waweze kukabiliana na mabadiriko ya ukusanyaji wa kodi ambapo JICA wataweza kuboresha mazingira ya ulipaji kodi ambayo huwa yanabailika kutokana na baadhi ya watu kukwepa kodi.
“Kimsingi lengo letu ni kuboresha huduma ya walipa kodi hivyo kuna moduli mbalimbali za mafunzo ambazo zitaweza kuwajengea uwezo wafanyakazi wetu,” alisema Bw. Kitillya.
Alisema ulipaji kodi ni wajibu wa kila mwananchi ili kuleta maendeleo kwenye serikali yake na kuwataka Watanzania kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari ili kuchochea maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA, Bw. Yukihide Katsuta, alisema mradi huo utakijengea uwezo wa kutoa mafunzo Chuo cha Kodi nchini (ITA) kwa wahitimu wake.
Alisema pia utasaidia kuimarisha mifumo ya kuandalia mafunzo, kuwaja uwezo wa wakufunzi wa chuo hicho na kuimarisha utaratibu wa mipango ya maendeleo chuoni hapo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment