26 July 2012

Kesi wizi wa nyara Kibiti kusikilizwa Agosti 22


Na Rose Itono, Pwani

MAHAKAMA ya Kibiti, iliyopo Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Agosti 22 mwaka huu, itaanza kusikiliza kesi ya kupatikana na nyara za Serikali inayomkabili mwendesha pikipiki 'bodaboda', Bw. Jumanne Ligenge na wenzake watano.

Kesi hiyo iliitwa juzi ambapo Hakimu wa Mahakama hiyo Bw. Muhidin Matitu, alisema jalada la kesi bado lipo kwa Mwendesha Mashtaka mkoani humo kwa uchunguzi zaidi.

Washtakiwa wengine ni Bw. Juma Libanga, Bw. Sanji Mwango, Bw. Omari Mpogo, Bi. Scola Mtumba na Bw. Bakari Mtango.

Awali Mwendesha Mashtaka wa kesi hiyo, Bw. Gabikwa Ushomile,  aliiambia mahakama kuwa, washtakiwa walikamatwa katika maeneo tofauti wilayani humo na nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa wa kwanza Bw. Ligenge alikamatwa Machi 30 mwaka huu Ikwiriri, akiwa amepakia meno ya tembo 42 kwenye pikipiki yenye namba za usajili T 557 ATL.

Washitakiwa wote katika kesi hiyo wako nje kwa dhamana hadi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa ambapo nje ya mahakama, baadhi ya wakazi wa Rufiji waliofika mahakamani hapo wameiomba Serikali kupitia mahakama kuharakisha usikilizwaji wa kesi za aina hiyo.

Bw. Hassan Nalonje, mkazi wa Rufiji alisema kuharakishwa kwa kesi hizo kutatoa fundisho kwa jamii yenye tabia hiyo.

Mkazi mwingine Bw. Abdallah Dilunga, alishauri vidhibiti vyote vikiwemo nyara za Serikali kutunzwa na Wizara ya Maliasili na Utalii badala ya mahakama ili kuimarisha ulinzi.

Hivi karibuni akiwa mjini Dodoma, Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Naibu Waziri Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii Dkt. Seif Sulemain Rashid, alishauri idara ya mahakama kuharakisha usikilizaji na uamuzi wa kesi zinazohusu nyara za Serikali.

Dkt. Rashid alishauri mahakama kutoa adhabu kali kwa watu wanaopatikana na nyara hizo pamoja na kuanzisha mahakama maalumu ili kukomesha tabia hiyo.

No comments:

Post a Comment