23 July 2012
Timu zetu kiwango bado Kagame
MICHUANO ya Kombe la Kagame ilianza kutimua vumbi Julai 14, mwaka huu ambapo tulishuhudia timu zetu za Tanzania zikianza michuano hiyo kwa kupepesuka.
Awali ilikuwa ni timu ya Yanga ambayo ilicheza na Atiletico ya Burundi na Yanga wakaambulia kipigo cha mabao 2-0, sambamba na Simba waliocheza siku inayofuata ambao nao waliambulia kipigo kama hicho kutoka kwa URA ya Uganda.
llikuwa ni ahueni kwa timu za Azam na Mafunzo ambazo zilianza kwa kutoa sare, na juzi pia Mafunzo ilitoa sare kutoka kwa Tusker ya Kenya.
Simba na Yanga walikuja kuzindukia kwa vibonde ambao Yanga waliibukia kwa Wau Salam ya Sudani Kusini na kujizolea mvua ya mabao 7-1, hali kadharika Simba nao siku inayofuata wakaifunga Ports ya Djibout.
Kwa viwango hivyo kwa timu zetu tunaweza kuishia katika hatua ya robo fainali, kwani huko timu zetu zitakutana na timu zenye uwezo mkubwa, changamoto iliyombele yao ni kuongeza bidii zaidi ili ziweze kufika mbali.
Mwaka jana naweza kusema timu zetu zilijiandaa vizuri kwani tulifanikiwa kuwaondoa wageni na fainali zikacheza timu zetu Simba na Yanga, ambapo Yanga ndio waliofanikiwa kulibakisha kombe hilo nyumbani.
Sasa mwaka huu tukicheza pia tunaweza kulipoteza kombe hili na kuchukuliwa na wageni, Watanzania hawapendi kuona kitu kama hicho, wanataka timu zetu zioneshe viwango na kufika fainali katika michuano hiyo.
Hivyo basi tunaziomba timu zetu ziongeze juhudi katika michuano hii ili kuwapa burudani wapenzi wa soka nchini na kutoa hamasa hata kwa wadhamini mwakani waweze kuifadhili michuano hii ili ifanyike tena hapa Tanzania.
Ni matarajio yetu tutaanza kuona soka la kuvutia na mabao mengi kutoka kwa timu zetu, kila la kheri timu zetu za Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment