23 July 2012

Kocha Wau Salaam atetea mabao 19 waliyofungwa


Na Speciroza Joseph

BAADA ya kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la Kagame yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kocha wa El-Salaam Wau Sebit Bol Chol amesema kukosa uzoefu kumeigharimu timu hiyo.


El-Salaam Wau katika mashindano hayo wamefungwa jumla ya magoli 19-1 katika michezo mitatu iliyocheza kwenye hatua ya makundi.

El-Salaam Wau walipoteza mchezo wa kwanza 7-0 kwa APR ya Rwanda, wakafungwa 7-1 na Yanga ya Dar es Salaam na juzi walifungwa 5-0 na Atletico ya Burundi.

Kocha wa timu hiyo kutoka Sudan Kusini, Sebit Bol Chol alisema wachezaji wake wamekosa uzoefu na kuruhusu kufungwa kiasi hicho cha magoli.

Alisema kupitia mashindano hayo wamejifunza vitu vingi ikiwemo maandalizi ya timu katika mashindano makubwa na wachezaji wake wamepata uzoefu utakaowasaidia katika michezo mbalimbali.

Akielezea sababu ya kupoteza michezo hiyo alisema, mchezo wa kwanza walikosa umakini, mchezo wa pili walianza kupata uzoefu na kuweza kutoa ushindani hasa kipindi cha pili.

"Mchezo na Atletico ulikuwa mgumu kwetu wachezaji watano walikuwa majeruhi pia na golikipa alikuwa majeruhi, hivyo tukamtumia mchezaji wa ndani awe golikipa lakini tunashukuru tumemaliza na kitu kipya vichwani kwetu" alisema Chol.

Kocha huyo aliongeza kuwa magolikipa wote wawili walipata majeruhi hali iliyosababisha kumtumia mshambuliaji Mubarak  Mohd Saleh ambaye alihimili mchezo huo na kufungwa magoli 5-0.

Akielezea muelekeo wa timu yake kocha Chol alisema watarekebisha makosa yote yaliyoonekana kwenye mashindano na kuahidi kufanya vizuri kwenye mashindano yajayo ya Kombe la Kagame wakiwa wanachamama wapya wa CECAFA.

No comments:

Post a Comment