11 July 2012

TFF yapigilia msumari wa mwisho wagombea Yanga



Na Zahoro Mlanzi

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeitaka Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Yanga, kuondoa majina manne ya wagombea walioshindwa kuwasilisha nakala za vyeti halisi kama ilivyoagizwa.


Wagombea hao ni Sarah Ramadhani (Uenyekiti), Zuberi Katwila, Yusuph Gao na Ramadhani Kampira (wote Ujumbe) ambapo sasa wameondolewa rasmi katika kinyang'anyiro cha uchaguzi huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwa niaba ya kamati hiyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema wamepokea barua ya maombi ya kupitia upya uamuzi waliochukua juu ya wagombea hao.

"Tulipokea barua hiyo na ikajadiliwa na kamati husika lakini baada ya kikao hicho, kamati hiyo iliyakataa maombi hayo kwani hayakuwa ya msingi kutokana na kamati hiyo iliambiwa kila kitu nini cha kufanya.

"Kamati iliagizwa kuhakikisha wagombea hao wanawasilisha vyeti vyao halisi vya elimu, lakini inaonekana wagombea hao hawakufanya walichoagizwa, hivyo wamevunja kanuni na tararibu za uchaguzi," alisema.

Akizungumzia mgombea mmoja mmoja, alisema Sarah hakutimiza masharti ambapo alitakiwa aambatanishe vyeti kitu ambacho amevunja kanuni ya 10,4,5 ya Ibara ya uchaguzi.

Alisema Katwila na Gao, wao vyeti vyao vilikuwa na utata ambapo NECTA iliagiza wapeleke vyeti halisi lakini wameshindwa kufanya hivyo na Kampira pia hakufanya hivyo.

Katibu huyo alisema kutokana na wagombea hao kushindwa kuwasilisha vyeti hivyo, imewaagiza Kamati ya Yanga kuwaondoa wagombea hao mara moja, ili kutoa nafasi zaidi kwa wagombea wengine kuendelea na kampeni.

Aliwapongeza wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwa utulivu waliouonesha katika mchakato mzima wa uchaguzi mpaka sasa na kuwataka waendelee hivyo hivyo mpaka watakapopata viongozi wapya Julai 15, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment