27 July 2012

TFF kuzichonganisha Simba, Yanga, Azam


Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeanza michuano mingine ya Super 8 kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza, ambayo itazikutanisha timu za Simba, Azam FC na Yanga ambazo zilishika nafasi tatu za juu katika ligi.


Simba ambayo ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu na Yanga zinadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro ambayo huzipa mishahara, vifaa vya michezo na fedha za kuandaa mikutano na za uchaguzi.

Michuano hiyo ambayo itaanza Agosti 4 hadi 18 mwaka huu, pia itashirikisha timu tatu za Zanzibar Super Falcon, Mafunzo na Jamhuri ya Pemba ambazo nazo zilishika nafasi za juu katika Ligi Kuu Zanzibar.

Mashindano hayo yatadhaminiwa na benki ya ABC ambayo itachezwa katika vituo vinne vya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar.

Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kuingia mkataba wa miaka mitatu kati ya TFF na benki hiyo Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah alisema michuano hiyo ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi za Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kutofanyika mashindano mara kwa mara kunachangia kwa kiasi kikubwa timu kuanza msimu mpya wa ligi kwa kusuasua, hivyo michuano hiyo itatoa nafasi kwa makocha wa kurekebisha kasoro za wachezaji wao kabla ya kuanza kwa ligi.

"Kutokuwepo kwa mashindano kunadidimiza viwngo vya wachezaji wa soka na ndiyo maana mwaka huu tuna mpango wa kurudisha michuano ya FA," alisema Osiah.

Alisema mbali ya kushirikisha timu tatu za juu za Bara na Zanzibar, pia michuano hiyo ya Supar 8 imetoa nafasi kwa timu mbili zilizopanda daraja kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambazo watazichagua zilizoonesha viwango vizuri katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza.

Katibu huyo alisema michuano hiyo itazisaidia timu hizo zilizopanda kupata uzoefu, kabla ya msimu wa ligi kuanza kwa kucheza na timu zenye uzoefu.

Alisema michuano hiyo itachezwa katika viwanja vya Shekh Amri Abeid, Amaani, CCM Kirumba na Uwanja wa Taifa ambapo kila timu itapata nafasi ya kucheza mechi kwenye viwanja hivyo.

Osiah alisema pia itasaidia kupunguza lawama za mashabiki wa soka ambazo zimekuwa zikitupiwa TFF, kuchezesha mashindano mengi Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi mkuu wa Benki ya ABC, Boni Nyoni alisema imedhamini michuano hiyo kwa mara ya kwanza, ikiwa na lengo la kuwazawadia wateja wake kwa kuwapa burudani ya soka.

No comments:

Post a Comment