27 July 2012
Yanga, Azam FC patachimbika kesho *Kiiza aipeleka fainali *Mtoto hatumwi sokoni
Na Speciroza Joseph
MABINGWA watetezi wa Kombe la Kagame, Yanga jana ilipenya hatua ya fainali baada ya kuifunga APR ya Rwanda bao 1-0 katika mechi ya nusu ya fainali ya michuano hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Yanga itakutana na Azam FC kesho katika mechi ya fainali itakayochezwa kwenye uwanja huo. Azam imeingia fainali hiyo baada ya kuifunga AS Vita mabao 2-1.
Mpira ulianza kwa nguvu, ambapo dakika 10 za mwanzo APR ilipesukuma mashambulizi ya nguvu kwa Yanga ambayo yalizimwa na kipa Ally Mustafa 'Bertez', ambaye aliokoa michomo mikali iliyopelekwa langoni kwake huku mkwaju mmoja ukigonga mwamba.
Dakika ya sita, Said Bahanunzi alipiga shuti fyongo lililotoka nje ya lango la APR ambayo ilijibu shambulizi hilo dakika ya nane, baada ya Leonel St. Preus kuachia shuti kali lililogonga mwamba wa goli.
Kiungo wa Yanga Athuman Idd 'Chuji', dakika ya 15 aliachia shuti la mbali ambalo hata hivyo liliokolewa na kipa wa APR, Ndoli Jean Claude.
Dakika ya 18, Selemani Ndikumana aliachia shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Yanga na kuwa kona tasa.
Kocha wa Yanga Tom Saintfiet, alifanya mabadiliko dakika ya 27 kwa kumtoa, Juma Abdul na kumwingiza Ally Shamte kwa lengo kupeleka mashambulizi langoni mwa APR baada ya kuona washambuliaji wake wanasuasua.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuingia na uchu wa kutaka kufunga, ambapo ilipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa APR, lakini mabeki walikaa imara kuondoa hatari zilizopelekwa langoni mwao.
Hata hivyo tatizo la Yanga lilikuwa katika kulenga goli, kwani mashuti mengi ya washambuliaji wake yalitoka nje.
Dakika ya 65 Yanga ilifanya shambulizi la nguvu lakini, Bahanunzi akiwa na kipa wa APR Claude alishindwa kufunga na mpira kuokolewa na mabeki.
Katika kipindi cha pili dakika ya 70 na 84 APR iliwatoa Danny Wagaruka na Leonel St. Preus, wakaingia Heriman Ngomirakiza na Barnabe Mubumbyi.
Kocha wa Yanga, Tom dakika ya 82 alifanya mabadiliko mengine baada ya kumtoa Shamte ambaye aliingia badala ya Juma na nafasi yake kuchukuliwa na Rashid Gumbo.
Mechi hiyo ilimalizika kwa suluhu na hivyo mwamuzi wa mchezo huo, Anthony Ogwayo kutoka Kenya kulazimika kuongeza dakika 30 za ziada.
Katika dakika hizo za ziada Yanga iliingia kwa mguvu na kupata bao dakika ya 99, lililofungwa na Hamis Kiiza kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na Haruna Niyonzima.
Dakika ya 104 mwamuzi, Ogwayo alimtoa nje Godfrey Taita kwa kadi nyekundu baada ya awali kuoneshwa kadu mbili za njano kwa kucheza rafu.
Katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa saa 8 mchana Azam FC ilitinga hatua ya fainali baada ya kuifunga AS Vita ya DRC Congo mabao 2-1. Mabao ya Yanga yalifungwa na John Bocco na Mrisho Ngasa wakti la Vita liliwekwa kimiani na Mfongang Alfred.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment