04 July 2012

TAZARA, Gema wadaiwa sugu NSSF


Na Gladness Mboma
 
SHIRIKA la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), linaongoza kwa kutowasilisha makato ya wafanyakazi wake sh. bilioni sita kwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ikifuatia Kampuni binafsi ya Ulinzi ya Gema inayodaiwa zaidi ya sh. milioni 900.

Mwanasheria wa NSSF, Bw. Selestine Ntagara, aliyasema hayo Dar es Salaaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika  Maonesho ya 36 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa.

Alisema ingawa kuna mashirika, kampuni na watu binafsi ambao wanadaiwa michango ya wafanyakazi wao, TAZARA na Gema ndiyo wadaiwa suguna.

“Tayari waajiri wake wamefikishwa mahakamani kwa sababu ya kutolipa makato ya watumishi wake kwa wakati, lengo letu si kuwashtaki bali tumelazimika kufanya hivyo kwa sababu wafanyakazi wanatudai sisi wakidhani waajiri wao wamelipa.

“Hadi sasa kuna kesi 28 mahakamani ambazo zinahusisha kampuni, mashirika na waajiri binafsi kutolipa makato wa wafanyakazi wao, nawaomba waajiri walete michango ya wafnyakazi ili kuepuka kufikishwa mahakamani,” alisema Bw. Ntagara.

Alisema waliofikishwa mahakamani kama watashindwa kulipa makato hayo, watafilisiwa mali zao kwa amri ya mahakama.

“Michango yote inapaswa kulipwa ndani ya mwezi mmoja, zaidi ya hapo mwajiri anatakiwa kutozwa asilimia tano ya kiwango ambacho  anatakiwa kutoa kwa mwezi,” alisema.

Bw. Ntagara aliongeza kuwa, wana imani TAZARA itaanza kulipa kwa sababu ipo chini ya Serikali, lakini Kampuni ya Gema kama itashindwa mali zake zitafilisiwa.

No comments:

Post a Comment