16 July 2012

TASWA yamzawadia mlemavu wa macho



Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimetoa kiasi cha sh. milioni moja kwa mwanamichezo mwenye ulemavu wa macho  Faudhia Chafungwe.

Faudhia alipewa fedha hizo na Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Hawa Ghasia juzi kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha baada ya kushinda kwenye mchezo wa riadhambio za mita 100 na 200 kwenye mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA).


Mchezji huyo ni moja ya wachezaji mbalimbali waliopewa zawadi kwa kufanya vyema kwenye michezo hiyo ambayo ilimalizika juzi kwenye viwanja hivyo vilivyopo wilayani Kibaha.

Zawadi hiyo ambayo ilikabidhiwa mchezaji huyo ambaye aliongozwa na ofisa elimu wa wilaya ya Mufindi Farida Mwasumilwe ilifurahiwa na mashabiki waliohudhuria ufungaji wa michezo hiyo.

Waziri Ghasia aliipongeza TASWA kwa kutoa zawadi hiyo na kusema wameonesha kuwa ni jinsi gani wanathamini michezo hasa kwa watu wenye ulemavu.

“TASWA wameonyesha mfano mzuri hasa ikizingatiwa waandishi wa habari ni kioo cha jamii hivyo kujitolea kuhamasisha jamii kushiriki michezo pasipokubagua ni hatua nzuri sana kwani wameungana na wadau wengine kuunga mkono kuendeleza michezo nchini,” alisema Ghasia.

Aliwataka wadau wengine nao wajitokeze kama walivyofanya TASWA na wengine kuunga mkono serikali katika kusaidia vipaji ambavyo vimeonekana, kwani hiyo ndiyo ya kuwapa morali ya kushiriki michezo.

Kwa upande wake ofisa elimu wa Mufindi Mwasumilwe naye aliishukuru TASWA kwa kuunga mkono michezo hasa kwa watu wenye ulemavu ili nao waweze kushiriki kama wale wasiokuwa na ulemavu.

Faudhia anasoma darasa la nne kwenye shule ya msingi Makalala wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, alikuwa kivutio kwenye michuano hiyo iliyofanyika kwa muda wa siku 10.

No comments:

Post a Comment