16 July 2012

Simba Vuvuzela kufanya sherehe kesho



Na Mwandishi Wetu

TAWI la Klabu ya Simba la Vuvuzela, limeandaa sherehe itakayohusisha wanachama, wapenzi wa klabu hiyo pamoja na wadau mbalimbali wa soka nchini, itakayofanyika Ukumbi wa Kuala Lumpa, Sinza kwa Remmy, Dar es salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa tawi hilo, Paulo Makoye, sherehe hiyo ni maalum kwa ajili ya kuchangisha fedha kwa ajili ya timu yao ya soka ya wanawake ‘Simba Queens’ inayoshiriki Ligi ya Soka Wanawake Mkoa wa Dar es salaam.

Alisema viongozi wakuu wa Simba pamoja na wadau mbalimbali maarufu wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo inayotarajiwa kuwa ya aina yake kutokana na maandalizi yake.

“Timu ya Simba Queens pamoja na kuwa inamilikiwa na makao makuu ya klabu ya Simba, lakini imezaliwa ikiwa chini ya tawi letu, hivyo kiutendaji bado mchango mkubwa imekuwa ikipata kutoka kwetu, hivyo tumeona tuitane na kuchangishana ili timu hiyo ishiriki vizuri na kutwaa ubingwa," alisema Makoye.

Alisema katika kunogesha sherehe hiyo baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza cha timu ya wanaume waliotwaa ubingwa msimu huu watahudhuria ikiwa ni kuwapa hamasa dada zao.

Makoye alisema mbali na kuchangisha fedha, pia watatumia nafasi hiyo kuzindua tawi lao kwa vile licha ya kuanzishwa mwaka mmoja na nusu uliopita na kuendelea kufanya kazi zake, lilikuwa halijazinduliwa rasmi.

Pia alisema, watatumia sherehe hiyo kuzindua tovuti ya tawi lao ambapo wanatarajia kuendesha mambo yao ya kiofisi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

No comments:

Post a Comment