30 July 2012
TAPOA wapata uongozi mpya
Na Frank Geofray, Jeshi la Polisi
CHAMA cha Askari Wastaafu wa Jeshi la Polisi (TAPOA), kimefanya uchaguzi wa viongozi wake ambao watakiongoza ili kufikia malengo ya kuchochea maendeleo ya wanachama.
Nafasi zilizogombewa katika uchaguzi huo ni Mwenyekiti, Mwenyekiti Msaidizi, Katibu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Mwanasheria wa chama, wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na wadhamini.
Katika uchaguzi huo, Bw. Hilary Rashid alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Bw. Mustapha Wangwi (Mwenyekiti Msaidizi), Chai Msugar (Katibu), Bw. Fadhili Walele (Katibu Msaidizi), SSP mstaafu Galimanywa (Mweka Hazina), ambapo Bw. Moses Lyimo ni Mwanasheria wa chama hicho.
Akizungumza baada ya kumalizika uchaguzi huo, Bw. Rashid ambaye ni Kamishna mstaafu wa Jeshi la Polisi, ametoa wito kwa askari wastaafu wa jeshi hilo kujiunga na chama hicho ili kiwasaidie kupata maendeleo na kudai stahiki zao.
Alisema hivi sasa ni wakati muafaka kwa wastaafu kujitokeza kwa wingi na kulisaidia Jeshi la Polisi katika kuimarisha dhana ya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii ili kupunguza uhalifu nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa TAPOA Bw. Msugar ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi mstaafu wa polisi, alisema umoja huo utawawezesha kukutana mara kwa mara na kubadilishana
mawazo na kushirikiana katika shughuli mbalimbali.
Alisema lengo la chama hicho ni kuhakikisha kinamfikia kila mstaafu popote alipo ili kupata wanachama wengi watakaoimarisha chama pamoja na kushirikiana na uongozi wa jeshi hilo.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Naibu Kamishna mstaafu wa polisi Bw. Abbas Mwamasoli, alisema changamoto waliyonayo ni kuhakikisha wanafika kila Mkoa kufungua matawi ili iwe rahisi kuwafikia wanachama wote walioostaafu wakiwa na vyeo mbalimbali bila ubaguzi wowote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment