30 July 2012

Sakata bei ya pamba kutua kwa Pinda


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

SAKATA la kushuka kwa bei ya pamba, limechukua sura mpya baada ya viongozi wa Halmashauri za Wilaya saba katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita, kuunda timu maalumu ya watu saba ambayo itakwenda kuonana na Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda.

Azimio la viongozi hao kutaka kuonana na Bw. Pinda lilifikiwa mwishoni mwa wiki kwenye kikao maalumu cha Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT), mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita (Bukombe) ambacho kililenga kujadili bei ya pamba na agizo la Serikali linalozitaka halmashauri kushusha viwango vya ushuru wa pamba.

Lengo la timu hiyo ni kumtaka Bw. Pinda aishauri Serikali ili iangalie uwezekano wa kuivunja Bodi ya Pamba nchini (TCB), baada ya kubainika imeshindwa kumsaidia mkulima wa zao la hilo badala yake imekuwa chanzo cha matatizo waliyonayo wakulima.

Katika kikao hicho, wajumbe wa ALAT kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu, walielezea masikitiko yao kutokana na serikali jinsi  ilivyoshindwa kusikiliza kilio cha mkulima wa zao la hilo baada ya kutangaza bei ya sh. 660 (kwa kilo moja ya pamba), ambayo itasababisha wakulima wengi wapate hasara.

Walisema Serikali inapaswa kuchukua uamuzi mgumu wa kukubali kutoa ruzuku kwa wakulima ili kufidia pengo la hasara ambayo wataipaata kutokana na kuuza pamba yao kwa sh. 660 na kutaka bei hiyo angalau ifike sh. 1,000 hivyo Serikali ikubali kuongeza sh. 340 kwa kila kilo kama fidia.

Wajumbe hao walipinga vikali agizo la Serikali kuzitaka halmashauri kupunguza kiwango cha ushuru wanachotoza kwa wanunuzi wa pamba kwa madai kuwa, hatua hiyo itasababisha halmashauri zipate hasara zaidi ya sh. bilioni  6.1 hivyo kushindwa kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa mwaka 2012/13.

Walisema mbali ya kushindwa kutekeleza mipango ya maendeleo, halmashauri pia zitashindwa kulipa mishahara ya watumishi wake.

No comments:

Post a Comment