06 July 2012

Tanzania yaziomba Marekani, EU kuchunguza meli za Iran



Na Goodluck Hongo

SERIKALI imeziomba nchi za Marekani na Umoja wa Ulaya (EU), kusaidia uchunguzi wa taarifa mbalimbali zinazohusu baadhi ya meli kutoka nchini Iran kupeperusha bendera ya Tanzania ili kukwepa vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa (UN).


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe, alisema taarifa hizo zimeanza kuchunguzwa ili kujua zina ukweli kiasi gani ambapo Tanzania pekee, haiwezi kufanikisha uchunguzi huo kwa sabbu meli hizo zinapita katika kina kirefu.

Alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Zanzibar, ilisema kuna meli 399 zilizosajiliwa na wakala kutoka kampuni ya Fellix ya Dubai na kati ya hizo 11 ni za mafuta.

“Tunazifanyia uchunguzi taarifa hizi, tunawaomba wenzetu wa Marekani na EU kusaidia uchunguzi kwani wao wana uwezo mkubwa zaidi kuhusu jambo hili.

“Kama itathibitika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Muunfano wa Tanzania, tutalimaliza kwa pamoja,” alisema.

“Tayari tumeijulisha UN, kuhusu ombi letu la kufanya uchunguzi, pia nilimuuliza Balozi wa Iran nchini lakini alikana, baadae nitakutana na mabalozi kuzungumzia jambo hili,” alisema.


Alisema lengo la kufanya uchunguzi ni kutokana na wakala huyo kukataa meli hizo sio za Iran, hivyo Tanzania kama wanachama wa UN, lazima isimamie makubaliano yaliyopo.

Bw. Membe alisema jibu la uchunguzi huo linaweza kutolewa wakati wowote na Serikali.

1 comment:

  1. TUWEKEZE KWENYE RASILIMALIWATU TUNAJITANGAZA SANA TUNA MADINI MENGI MAENDELEO HAKUNA HIYO SI HOJA MBONA CONGO INAMADINI MENGI WALA HATUFUI DAFU LAKINI NI YA MWISHO KIUCHUMI DAWA NI KUWA NA RASILIMALI NDIO UFUMBUZI WA UCHUMI DUNI

    ReplyDelete