06 July 2012

Aanguka mtini wakati akitaka kuvuna asali



Na Thomas Kiani, Singida

MKAZI wa Kijiji cha Mgungia, Kata ya Kaselya, Wilayani Iramba, mkoani Singida, Bw. Godfrey Athumani (51), amenusurika kufa baada ya kuanguka na tawi la mti lililokuwa na mzinga wa nyuki.

Wakizungumza na Majira jana, Bw. Jeremia Athumani na Bw. Samweli Kitamawe ambao ni ndugu wa Bw. Athumani, walisema tukio hilo limetokea juzi, saa tatu usiku, kijijini hapo.

Alisema Bw. Athumani alikwenda shambani kwake na watu wanne kuvuna asali katika mizinga yake kwa matumizi ya nyumbani.

“Walipofika kwenye mizinga wakati wanajiandaa kutengeneza moto, Bw. Athumani alipanda juu ya mti akiwa na kamba mkononi hadi kwenye tawi lenye mzinga na kuanza kuufunga.

“Wakati akiuweka sawa ili ashuke nao taratibu, tawi lenye mzinga likakatika baada ya kuzidiwa na uzito, mzinga ulitangulia chini na yeye kuangukia juu yake hadi akachanika uso, kuvunjika mkono wa kushoto na kuzimia papo hapo,” walisema.

Waliongeza kuwa, nyuki waliokuwa ndani ya mzinga huo walitoka na kuanza kumshambulia Bw. Athumani kabla moto huo haujawaka vizuri lakini wenzake waliweza kumvuta na kumkimbiza nyumbani ambapo baadae alizinduka.

“Nakumbuka nilidondoka na tawi lakini baada ya hapo sikumbuki nini kilitokea hadi nilipokuja kujikuta nipo nyumbani pamoja na maumivu makali ya mkono, uso na kifua,” alisema Bw. Athumani.

Alisema ndugu zake walimchukua na kumkimbiza Hospitali ya Mkoa ambako alishonwa nyuzi nane usoni na kufungwa bandeji gumu 'POP', Katika mkono wa kushoto ambao ulivunjika.

Katika tukio jingine, wiki iliyopita mkazi wa Kijiji cha Irisya, Singida Vijijini, Bw. Imanuel Shankana (75), amefariki dunia baada ya kuanguka kwenye mti na mzinga wa nyuki ambao alishindwa kuumudu kutokana na uzito wake akiwa amelewa pombe.

No comments:

Post a Comment