16 July 2012

TANESCO yaanza msako wa kuwanasa wezi wake



Na Willbroad Mathias

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limeanzisha operesheni maalumu katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha linavunja mtandao wa wezi wa umeme.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Meneja Mahusiano kwa Umma wa shirika hilo, Bi. Badra Masoud, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuibuka kundi la watu ambao wanauza umeme wa LUKU bila kuunganishwa na shirika hilo.


Alisema kwa kipindi kirefu, mtando huo umekuwa ukifanya shughuli hiyo bila kujulikana na kusababisha shirika kupata hasara.

“Kwa sasa tupo katika operesheni kabambe ya kuhakikisha tunavunja mtandao huo kwani unalitia hasara shirika letu, pia kuna wizi unafanywa na baadhi ya wateja wasiokuwa wa amini wanaochezea mita za LUKU,” alisema.

Alisema matukio hayo ndiyo yamewafanya kupita nyumba hadi nyumba ili kukagua mita na kufanikiwa kuwanasa watu kadhaa wakiwa na umeme mwingi tofauti na manunuzi yao.

Aliongeza kuwa, shirika hilo lina uwezo wa kutambua matumizi ya mtumiaji wa nishati hiyo tangu aliopofungiwa mita ya umeme.

“Hata kama ulifungiwa mita mwaka 2000, shirika lina uwezo wa kutambua kiasi cha umeme ulionunua tangu kipindi hicho hivyo kama uliichezea mita lazima tutakubaini,” alisema na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa shirika hilo ili kuhakikisha wanaolihujumu wanafikishwa mahakamani.


No comments:

Post a Comment