16 July 2012
Serikali yapewa muda wa kutoa majibu madai ya walimu
Na Darlin Said
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimeitaka Serikali kutoa majibu ya madai ya walimu kabla ya Julai 23 mwaka huu, ambayo yanahusu ongezeko la mishahara kwa asilimia 100 na posho mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es alaam jana, Rais wa chama hicho, Bw. Gratian Mukoba, alisema wameamua kutoa msimamo huo baada ya Serikali kuomba waongezewe muda ili waweze kutekeleza madai yao.
Alisema awali walikubaliana na Serikali kutekeleza madai hayo Julai 10 mwaka huu na baada ya kukutana, waliomba kuongezewa muda ambapo CWT, kimeongeza muda huo hadi Julai 23 mwaka huu, Serikali iwe imetoa tamko juu ya madai hayo.
Bw. Mukoba alisema, mikakati mbalimbali imepangwa kuwavuruga walimu ili washindwe kudai haki zao pamoja na kuwadanganya wananchi kuwa mgogoro wa walimu unachochewa na wanasiasa.
Aliongeza kuwa, mkakati mwingine ni kuwatishia walimu kuwa watafukuzwa kazi na kuhakikisha hawapati taarifa zinazotolewa na CWT kama njia pekee ya kuwazuia wasidai haki zao.
Bw. Mukoba alikanusha kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bw. Kassim Majaliwa kuwa walimu hawajatangaza mgogoro na Serikali wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika, aliyetaka Serikali kutoa tamko ni lini watamaliza mgogoro wake na walimu.
“Nimesikitishwa na kauli hii kwa kuwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Celina Kombani, alishatoa tamko kwa Watanzania kuwa, CWT kimesajili mgogoro wake kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.
“Pia Kamishna wa Kazi katika taarifa yake kwenye vyombo vya habari, aliwajulisha Watanzania juu ya mgogoro huu,” alisema Bi. Kombani
Bw. Mukoba alisema, chama hicho kinashangazwa na kauli tofauti zinazotolewa na Serikali na hakukuwa na kiongozi yeyote bungeni aliyekuwa tayari kusahihisha upotoshaji huo.
Hata hivyo, CWT kimetoa wito kwa Serikali na viongozi husika, kuwaeleza Watanzania juu ya mgogoro uliopo kupitia Bunge.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment