26 July 2012

SUMATRA yaigomea TPA kupandisha tozo


Na Anneth Kagenda

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA-CCC), limeigomea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), kuhusu ombi lao la kuongeza tozo mbalimbali za kuhudumia meli.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, katika mkutano wa wadau uliolenga kujadili mapendekezo ya TPA kuhusu ongezeko hilo, Katibu Mtendaji wa CCC, Bw. Osca Kikoyo, alisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha biashara kuyumba na wadau kukimbia.

Alisema TPA haiwezi kupandisha tozo kwani kufanya hivyo kunaweza kuwafanya wadau kukimbia pia kuna vitu ambavyo havijaainishwa na kueleza wapi wanapata hasara au faida.

“Mamlaka hii pamoja na kutaka kupandisha tozo za meli, hawajasema hasara kiasi gani wanapata au wanafaidika vipi, tangu mwaka 1998-2012, wako kimya leo wanataka kupandisha tozo asilimia 17 hadi 132, sisi tumegoma haiwezekani,” alisema.

Alisema katika maombi yao, TPA imekiuka kanuni ya SUMATRA na zile za uwasilishaji nauli kipengele cha sita, kipengele kidogo cha kwanza ambacho kinamtaka mleta apeleke maombi yanayoonesha viwango vilivyopo na kama wanaingia hasara kwa kiasi gani.


Kaimu Mkurugenzi wa Masoko TPA Bi. Francisca Muindi, alisema lengo ni kuangalia uwezekano wa kuongeza tozo kwa wenye meli  ambapo hoja kuu ni kupandisha tozo ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

“Majukumu yetu  ya kuendesha bandari na miundombinu yake ni makubwa hivyo fedha tunayopata, ndio hiyo tunayoendeshea kazi zetu,  huwezi kusema TPA iendelee kutoza kiasi hicho wakati natakiwa nitumie uchumi wa kijografia,” alisema Bi. Muindi.

Alisema gharama za meli awali zilikuwa ni dola za Marekani 4.15 ambapo ombi lao ni kuitaka SUMATRA ipendekeze na kufikia dola saba.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Bw. Ahmad Kilima, aliwakumbusha watumiaji wa bandari kwamba wasigeuze eneo la PTA kuhifadhi shehena zao kwani bandali ni mlango wa kupitia shehena sio kuhifadhi.

No comments:

Post a Comment