26 July 2012

Mradi wa uboreshaji makazi Manzese wamgusa Tibaijuka


Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema miradi ya uboreshaji makazi nchini haiwezi kufanikiwa bila kushirikisha sekta za kibenki kwani wananchi hawawezi kununua kwa fedha kutoka mifukoni mwao.

Prof. Tibaijuka aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa Benki ya Azania nchini ambayo imetoa mkopo wa sh. milioni 65 kwa ajili ya mradi wa mikopo ya kuboresha nyumba (TAFSUS).

Mradi huo utahusisha kaya 15, zilizopo Manzese, Kata ya Mvuleni, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba ili waweze kujipatia makazi.

“Mradi huu umelenga kuboresha makazi katika Wilaya hii, mwananchi pekee hawezi kununua nyumba kwa fedha kutoka mfukoni mwake bila kushirikisha mabenki.

“Naipongeza benki hii kwa ushirikiano waliotoa katika mradi huu kwa kujitokeza kuudhamini, lengo si kuboresha makazi ya watu wa Manzese pekee, bali nchi nzima kwa ujumla,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya TAFSUS, Bw. Salmoni Odungo, alisema mikopo iliyoidhinishwa kwa ajili ya mradi huo ni zaidi ya sh. milioni 457.3 na kuipongeza benki hiyo kuwa ya kwanza kuthubutu kushiriki mradi wa uboreshaji makazi na kuzitaka taasisi nyingine za fedha kuiga mfano huo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Charles Singili, aliwataka wananchi kuendeleza utaratibu uliooneshwa na wakazi wa Mvuleni wa kujiunga kwenye vikundi na kwenda TAFSUS kuomba mikopo.

“Tunawaomba wananchi wengi wathubutu kama zilivyofanya kaya 15 za Mtaa wa Mvuleni kwa kuthubutu na kujiunga kwenye mpango huu ili tuwe mfano wa kuigwa nchini na duniani, kuunganisha nguvu zetu tunaweza tukabadilisha makazi yetu,” alisema Bw. Singili.

Alimshukuru Prof. Tibaijuka kwa ushirikiano aliowapa akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi Duniani (UN-Habitat), kwa kuhakikisha benki hiyo inajipanga na kutoa mkopo huo ili kuuwezesha mradi kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment