20 July 2012

Spika Makinda atupiwa tuhuma nzito



Rehema Maigala na Stella Aron

CHAMA cha Alliance For Democratic Change (ADC), kimedai kusikitishwa na kitendo cha Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda kukataa kuhairisha kikao cha Bunge baada ya wabunge kupata taarifa za kuzama kwa meli ya Mv. Skagit, karibu na Kisiwa cha Chumbe, visiwani Zanzibar.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Said Miraji, alisema hatua hiyo iliwashangaza wananchi wengi waliokuwa wakiangalia kikao cha Bunge kwa njia ya televisheni pamoja na wabunge wenyewe.

Alisema ombi la Mbunge wa Wawi, Bw. Hamadi Rashid Mohamed (CUF), kutaka kikao cha Bunge kisitishwe kutokana na taarifa za maafa hayo, lilipaswa kupewa uzito wa pekee

“Sisi ADC tumesikitishwa na hatua ya Bi. Makinda kutokubali ombi la Bw. Mohamed mara moja, hoja yake ilikuwa na maani kubwa badala yake Bw. Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), ndiye aliyesikilizwa, busara haikutumika,” alisema.

Bw. Miraji aliwapongeza wabunge wa Zanzibar na wale wa upinzani kwa kuamua kutoka nje ya ukumbi wa Bunge kabla Bi. Makinda hajaahirisha kikao hicho na kusisitiza kuwa, wabunge hao wameonesha ni jinsi gani wanavyowajali wapiga kura.

“Umefika wakati wa Bi. Makinda kutumia busara hasa linapotokea tatizo au taarifa ambazo si nzuri kwa Taifa letu hivyo kusoma alama za nyakati,” alisema Bw. Miraji na kuongeza kuwa, kutokana na ajali hiyo, chama hicho kimeshusha bendera zake nusu mlingoti  nchi nzima ili kuungana na Serikali katika kipindi hiki kigumu.

Katika hatua nyingine, Bw. Miraji aliishauri Serikali kuwa na mikakati maalumu ya ukaguzi wa vyombo vya majini mara kwa mara ili kuepusha ajali zinazotokea.

Alisema hivi sasa matukio ya kuzama kwa meli nchini yamezidi kuongezeka hali inayochangiwa na kutofanyiwa ukaguzi hivyo ni bora wananchi walalamikie ukosefu wa usafiri badala ya kuendelea kupoteza maisha.

“Tanzania haina uwezo wa kukabiliana na majanga kwa sababu hatuna vifaa vya uhakika,” alisema.

Pamoja na madai ya NDC, Mwandishi Benedict Kaguo kutoka Dodoma anaripoti kuwa, juzi Bi. Makinda alitoa ufafanuzi wa jambo hilo kwa wabunge na kusema kuwa, Bunge lisingeweza kuhairishwa kwani walikubaliana Serikali itatoa kauli baada ya kuwasiliana na mamlaka husika Zanzibar ili kupata taarifa rasmi.

Baada ya maelezo hayo ambayo aliyatoa ndani ya Bunge, wabunge wote wa CUF na upinzani waliamua kutoka nje wengine wakiangua vilio nje ya ukumbi ambapo Bw. Mohamed, aliitisha kikao cha dharua cha wabunge ili kuangalia namna ya kwenda Zanzibar.

Dkt. Nchimbi alitoa hoja ya kusitisha kuendelea na hotuba ya bajeti ya Wizara yake ambapo kutokana na hali hiyo, Bunge lilihairishwa kupitia kifungu cha 58(5).

Wabunge wa Zanzibar walilalamikia uamuzi wa Bi. Makinda kuzuia hoja ya Bw. Mohamed na kushauri kuwa baada ya kurudi bungeni, upo umuhimu wa kupiga kura ya kumkataa ili kumuondoa katika nafasi hiyo kwa madai kushindwa kuongoza Bunge hasa panapotokea dharura kama hiyo.

Mbunge wa Mji Mkongwe, Bw. Mohamed Sanya, alisema kitendo cha Bi. Makinda kuzuia hoja ya mwenzao ni dharau kubwa kwani mbunge anapofariki ghafla Bunge huahirishwa lakini wanapokufa wapiga kura bunge liendelee.

“Haina maana ya mimi kuwa mbunge, Spika anaambiwa kuna watu zaidi ya 200 wamezama baharini na yeye kusema hiyo si hoja ya dharura...marehemu Amina Chifupa alivyokuwa Bunge lilihairishwa, mbunge ana thamani gani kama walionileta hapa hawathaminiki,” alisema Bw. Sanya huku akitokwa machozi.

3 comments:

  1. Huyo Mama yenu makinda ya ndege hajalichochote si wanaccm wapo wanaomsapoti????huyo ni kumpiga chini.Watu wanakufa yeye anaona sawa tu mpumbavu sanan huyo mwananke makinda ya ndege.

    ReplyDelete
  2. Kwa kweli Anna Makinda natakiwa kuachia ngazi ya uspika. Ameonesha kutokuwa na jamii iliyomfikisha alipo na kujali maslahi ya watu wachache na hasa waliomfikisha alipo. Hatakiwi kuongoza tena jamii, na kama wabunge wataendelea kuwa naye kama spika wao basi na hilo bunge halitakuwa na maadili yake, ni kuwa wanaburuzwa na waoga wa kupoteza nafasi waliyo nao, wakati huo huo waliowachagua wakipoteza imani nao.

    ReplyDelete
  3. NI WENYE UFINYU WA UELEWA WANAWEZA KUSEMA WATAKAVYO VIKAO VYA BUNGE VINAONGOZWA KWA KODI ZA WANANCHI SINA UHAKIKA MAMA MAKINDA NDIYE ANAYEWAPA WABUNGE POSHO TUACHE UJINGA LAZIMA AWASILIANE NA VYOMBO VINGINE KUTENGUA RATIBA YA BUNGE KWANI ANAUWEZO WA KUONGEZA BUDGET YA BUNGE TUACHE UFINYU WA MAWAZO KILA MTU AKINYAMAZA SI RAHISI KUJUA MTU ASIYE NA BUSARA JITAHIDINI KUTOFAUTISHA RASILIMALIMTU NA MTU WATU WENGI WANA UTAJIRI WA NYAMA ILA WANA UMASKINI WA MIFUPA

    ReplyDelete