16 July 2012
Sanaa inaweza kujenga madili
MKURUGENZI wa Utafiti,Mafunzo na Habari wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw Godfrey Mngereza amesema Ujio wa Sayansi na Teknolojia umepokelewa kwa mtazamo hasi hasa kwa Watoto na Vijana badala ya kuleta maendeleo na Utaifa kama ilivyotarajiwa na watanzania wengi.
Akitoa mada kwa madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro hivi karibuni kuhusu Matumizi ya Sanaa kama nyenzo ya kufundishia mashuleni, Bw Mngereza alisema kuwa maadili ya watoto wetu yameporomoka kutokana na kuacha kudhibiti uhuru wa teknolojia hasa ya Televisheni na hivyo watoto kuiga mambo yasiyofaa katika jamii.
Amesema wafanya maamuzi kama walivyo madiwani hao ni lazima wachukue hatua kuhakikisha maadili haya yanarudi kwa kutumia sanaa kuleta maendeleo,lakini pia kama nyenzo na njia ya kufundishia na kwa hiyo kuna haja pia ya kuwajengea uwezo wa kutosha walimu wa shule za msingi ili kufanikisha hatua hii muhimu.
Katika Semina hiyo ambayo iliandaliwa na Ngoma Afrika kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ina lengo la kuwapa uelewa juu ya mradi wa PAUKWA ambao kwa pamoja unatekelezwa kati ya Ngoma Afrika na Halmashauri hiyo na nafasi ya madiwani katika kuwaelimisha wazazi na wananchi kwa ujumla ni jinsi gani sanaa inaweza kuwasaidia watoto na hasa wa shule za msingi kujifunza masomo mbalimbali na maadili.
Bw Mngereza alisema miaka ya nyuma sanaa iliwajenga vijana kimaadili, lakini kwa sasa maadili yameporomoka na ni lazima juhudi zifanyike kupitia sanaa ili kurekebisha maadili haya na kwamba mwalimu ana nafasi kubwa sana ya kumjenga mtoto kwa hiyo lazima ajengewe uwezo wa kutekeleza jukumu hili la msingi.
“Madiwani kama watunga sera na wasimamizi wa utekelezaji wake je mnatenga bajeti kwa ajili ya sanaa na kuwajengea uwezo watoto ili kulinda maadili yasiporomoke,” alihoji Bw Mngereza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ngoma Afrika Bw Davie Kitururu mapema alibainisha kuwa mradi huo wa PAUKWA ni wa Manispaa ulianza na shule mbili za msingi za Albert Luthuli na Bungo lakini kwa sasa unashirikisha shule za msingi 20 lakini changamoto iliyopo ni uelewa wa wazazi,madiwani na wananchi kwa ujumla juu ya dhana hii ya kutumia sanaa kama nyenzo muhimu ya kufundishia.
Alisema madiwani lazima waifahamu dhana hii ili ifike kwa wananchi wakati wanapojadili mambo mbalimbali ya maendeleo na watenge bajeti kwa ajili ya mradi huu na kwamba pamoja na ufadhili uliopo kutoka Denmark lakini lazima pia Halmashauri ichangie ili uweze kufanikiwa na baadae usambae mkoa mzima.
Akifungua mafunzo hayo Meya wa Manispaa ya Morogoro Mstahiki Amir Nondo alisema mradi huu ni matokeo ya mahusiano yaliyokuwepo kati ya Manispaa ya Morogoro na nchi ya Denmark wakati wa utekelezaji wa mradi wa awali wa SUMO na akasisitiza ni lazima fedha zitengwe kwa ajili ya mradi huu wa PAUKWA ambao ki msingi ni mradi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
“Mradi huu ni utekelezaji wa ilani ya kutambua vipaji na kuviendeleza ili kukuza wigo wa ajira kwa vijana lakini pia kujenga maadili kwa vijana wetu kupitia sanaa,” alisisitiza Meya huyo.
Alibainisha kuwa sehemu ya mapato yatakayopatikana kutoka katika kituo kikuu cha mabasi Msamvu itatumika kusaidia Mradi huu wa Sanaa kama nyenzo ya Wanafunzi kujifunzia na kwamba hii ni fursa kwa madiwani kuulewa mradi huu ili waweze kuutekeleza na kuufikisha kwa wananchi ili wautambue kuwa una lengo la kuwakomboa watoto wetu kutokana na kuporomoka kwa maadili,njia mbadala ya kufundishia na pia kukuza vipaji na wigo wa ajira kupitia sanaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment