11 July 2012

Simba, Azam kucheza fainali Dar



Na Speciroza Joseph, Zanzibra

KAMATI ya Maandalizi ya Mashindano ya Urafiki Tanzania, imekubalina na ombi la timu za Simba na Azam FC kuhamishia fainali za mashindao ili kuchezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Fainali hizo zilipangwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa, lakini kutokana na mabadiliko hayo fainali hizo sasa zitachezwa Dar es Salaam kesho.

Kamati ya mashindano hayo, iliombwa na timu hizo kuupeleka mchezo huo kwenye uwanja mwingine na hata kama ni Pemba, lakini kamati hiyo ikasema gharama zitakuwa kubwa kwa kuwa klabu hizo zilitaka kwenda na ndege na si kutumia usafiri wa maji.

Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Amani Makungu alisema wamesikitishwa na hatua ya klabu hizo kuchukua maamuzi hayo kwa kuwa yanaharibu mipango yote ya maandalizi ya mashindano hayo.

"Tumesikitishwa na maamuzi ya Simba na Azam FC kwa kuwa mechi zote wamecheza katika Uwanja wa Amaan, kukataa mchezo wa fainali halikuwa jambo jema kwetu," alisema Makungu.

Aliongeza kuwa lengo la mashindano hayo ni kujenga uhusiano mwema kati ya Watanzania Bara na visiwani, kama wangejipanga mapema wangebadilisha lakini kwa sasa hivi matayarisho yote yameshafanyika.

Maombi ya klabu za Simba na Azam FC yalichukua zaidi ya saa nne kujadiliwa na mwisho kupelekwa kwa Waziri wa habari, Utalii na Michezo, Zanzibar kujadiliwa na kutolewa maamuzi ya mwisho.

No comments:

Post a Comment