09 July 2012

Simba, Azam kazi moja leo Z'bar



Na Speciroza Joseph, Zanzibar

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba leo watashuka uwanjani kucheza dhidi ya Zanzibar All Stars kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali ya michuano ya Urafiki Tanzania ,inayoendelea kwenye Uwanja wa Amaan,
Zanzibar.


Simba itacheza mchezo huo ikiwa imeshinda michezo miwili na kutoka sare mmoja katika hatua za makundi, endapo ikishinda itacheza na mshindi kati ya Azam na Super Falcon katika fainali itakayochezwa Jumatano.

Michuano hiyo yenye lengo la kudumisha urafiki na ujirani mwema kwa Tanzania bara na visiwani ilianza wiki iliyopita na kuhusisha timu nane, tatu kutoka bara na tano kutoka Zanzibar, kabla ya kuondolewa Klabu ya Yanga.

Simba inatumia wachezaji wake wote wa zamani na wale waliosajiliwa hivi karibuni katika kikosi hicho ikiwa ni sehemu ya kujipima na kuandaa kwa ajili ya kushiriki Kombe la Kagame.

Endapo vilabu hivyo vya kutoka bara vikishinda kwenye michezo ya nusu fainali zitakutana tena kwenye fainali, kama ilivyokuwa katika hatua za makundi ambao Simba na Azam FC zilikutana na timu hizo kutoka sare ya 1-1.

Kocha wa Simba Milovan Cirkovic, alisema kuingia nusu fainali ya mashindano hayo ni nafasi kwa wachezaji wake kupata uzoefu na kujiandaa hivyo kushinda katika mchezo huo ni sehemu ya maandalizi na muhimu kwao.

Naye Kocha msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala alisema wameweza kushinda na kuingia nusu fainali na huu ni wakati wao kucheza na kushinda mchezo dhidi ya Falcon ili waingie fainali hizo.

Timu za Jamhuri, Mafunzo na Zanzibar U23 zilitolewa katika hatua za makundi kwa kuwa na pointi chache.

No comments:

Post a Comment