09 July 2012

"Kupata medali Olimpiki ni ngumu'


Na Amina Athumani, Zanzibar

WAKATI ahadi ya sh. milioni 13.2 ikiahidiwa kutolewa kwa mwanamichezo atakayetwaa medali katika michuano ya Olimpiki itakayofanyika London, Uingereza, Mdau wa michezo nchini, Noeli Kiunsi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha kuogelea Tanzania (TSA), amesema ni vigumu kupatikana medali katika michuano hiyo labda ziwepo nguvu za miujiza.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu akiwa Dar es Salaam jana , Kiunsi alisema ni ukweli kwamba hiyo ni changamoto kubwa sana waliopewa wanamichezo hao kwa kuwa michezo hiyo ni migumu.

Alisema wapo wanamichezo wengi wazuri kutoka nchi mbalimbali ambao wana uzoefu mkubwa kuliko wanamichezo wa nchini na kwamba dua za watanzania zinahitajika ili kuwasaidia wanamichezo hao waweze kufanya vyema .

Alisema kwa upande wa muogeleaji ambaye wameweza kumuandaa kwa ajili ya michezo hiyo ya Olimpiki ambaye atacheza muundo huru wa meta 100 atashindana na wanamichezo zaidi ya 205  kutoka nchi mbalimbali.

Alisema pia kwa upande wa ngumi na riadha hali ni hiyo hiyo ambapo wanategemea kushindana na wanamichezo zaidi ya 100 na kwamba medali zinazowaniwa katika makundi yote ni medali tatu jambo ambalo ni changamoto kubwa  na itakuwa ni kazi ngumu sana kwao.

Alisema wanapongeza ahadi hizo zilizotolewa na wadau hao wa michezo na kwamba zitaweza kuwapa morali wanamichezo hao kwa kujitahidi watakapokuwa uwanjani wakati wa kulipigania taifa lao.

Alisepa pia Serikali ilitakiwa kuonesha moyo wao kwa wanamichezo hao kwa kuahidi chochote ambacho pia kingeweza kuwapa morali wachezaji hao watakapokuwa wakipigania nchi yao katika michuano hiyo.

Timu hiyo ya Tanzania iliondoka nchini jana, kwenda London kwa ajili ya michuano hiyo iliyopangwa kuanza Julai 27, mwaka huu ambapo wametangulia kwenye jiji hilo kwa ajili ya kupiga kambi ya mazoezi kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.

Wanamichezo watakaoiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo ni Zakia Marisho, Samson Ramadhan, Msenduki Mohamed na Faustin Musa ambao ni wanariadha, Selemani Kidunda ambaye ni bondia na Magdalena Moshi ambaye ni muogeleaji.

No comments:

Post a Comment