23 July 2012

Shibuda aichana serikali ya CCM



Na Benedict Kaguo, Dodoma

MBUNGE wa Maswa Mashariki, mkoani Shinyanga, Bw. John Shibuda (CHADEMA), amesema nchi inaongozwa kwa misingi ya Mabepari na kusababisha Watanzania maskini kutengwa na maendeleo kwa sababu CCM haipo madarakani


Bw. Shibuda aliyasema hayo mjini Dodoma jana wakati akizungumza na Majira kuhusu utoro wa wabunge ambao wengi wao kutoka chama tawala CCM, kukwamisha upitishaji Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa, CCM ambayo waliiamini kuongoza Serikali, haiko madarakani bali Serikali inajiongoza yenyewe kwa kutumia mifumo ya Kimagharibi badala ya msingi wa kuanzishwa kwa chama hicho.

“Serikali hii inasema wawekezaji kwanza, kilimo nyuma ikitumia nembo ya CCM wakati ukweli ni kwamba, Serikali imeitenga misingi ya kuanzishwa chama chao, sawa na gari ambayo imetengenezwa China na kuwekwa nendo ya Uingereza.

“Shabaha na malengo ya kudai uhuru wa Tanganyika ilikuwa kujenga misingi ya ustawi na maendeleo ya jamii, Taifa kushika hatamu za uchumi kwa masilahi ya uhuru ni maendeleo kwa taifa..dira hii ndio iliyoisukuma Tanzania kuunga mkono madai ya uhuru na ukombozi,” alisema Bw. Shibuda

Aliongeza kuwa, kwa misingi hiyo wananchi wa kawaida wataendelea kubaki maskini ndio maana wakulima wanateseka na bei ya mazao likiwemo pamba kutokana na Serikali kuwasahau.

“Serikali inatekeleza siasa na sera za huisho la kufufua umangimeza na mabwenyenye, wamewageuza Watanzania malighali ya huduma ya utwana wa maisha bora Ulaya.

“Uthibitisho juu ya hili ni mikataba mibovu inayopora rasilimali za nchi...maliasili za Tanzania zimechomwa mikuki ya mirija ambayo inafyonzwa na wawekezaji, Taifa linabaki na kuimba wimbo wa kazi ya mungu haina makosa kumbe ni kazi shetani Mungu tunamuonea,” alisema Bw. Shibuda.

Alisema inashangaza leo hii kuona mbunge akipewa Uwaziri, anabadilisha mienendo yake na kuwasahau walalahoi ambao ni Watanzania wanaotegemea kuongozwa.

Bw. Shibuda alisema CCM inapaswa kuwa baba wa kuingoza Serikali ambayo siasa na sera zake, zimetelekezwa katika makabati ya vitabu.

“Serikali hii sawa na chui aliyevaa ngozi ya kondoo...ukiona ngozi unajua ni ujamaa na kujitegemea kumbe ni mzimu wa chui ambao unateketeza rasilimali na maliasili kwa mapambio ya kuwaita wawekezaji, rasilimali zetu zinapelekwa nje na mabebari.

“Thamani ya rasilimali ndio bima ya maisha bora kwa kila Mtanzania na mkulima wa pamba, nchi haitaweza kusunga mbele kwa dhamira ya kuwa na Taifa huru la ujamaa na kujitegemea kwa sababu vitendo vya viongozi kuongoza njia ya safari ya kufaidi uhuru na maendeleo na kujitegemea,” alisema.

Alisema viongozi wana tabia na matendo yasiyokubalika hata na dini zao hivyo Watanzania wanajazwa ujinga wa hewala si utumwa kwa dhana ya utandawazi unaobarikiwa na vifuniko vya diplomasia za uchumi ambazo ni nusu kaputi za kulala usingizi.

2 comments:

  1. WABUNGE MUWAHESHIMU WATANZANIA MUNATUMIA KODI ZETU KULIPWA POSHO BUNGENI HAINGII AKILINI NYIE KUSISTIZA KILA MRADI UPIMWE UBORA KUTOKANA NA FEDHA ZILIZOTUMIKA INAKUAJE MUNATOROTOKA BUNGENI LAKINI MUNADAI POSHO MUKO KIMASILAHI ZAIDI KULIKO KUTETEA WATANZANIA ILA MTAPIMWA KUTOKANA NA AHADI ZENU KWA UMMA KUTOKUTEKELEZWA TUTAKUTANA 2015

    ReplyDelete
  2. HAO WABUNGE WATORO watajwe kwa majina na majimbo waliotoka ili wananchi tuwafahamu. 2015 tuc wachague tena. lengo kutu wakilisha. kama wana buss zao bac demoklasia itumike 2015

    ReplyDelete