02 July 2012

Serikali yatakiwa kutoa elimu ya sensa,katiba kwa wananchi


David John na
Goodluck Hongo

KUFUATIA Taifa kukabiliwa na michakato mitatu ya vitambulisho vya utaifa,sensa, na katiba mpya wadau mbalimbali wamezitaka mamlaka zinazohusika kutoa elimu thabiti kwa wananchi ili kuweza kushiriki kikamilifu michakato hiyo.

Wadau hao wametoa kauli hiyo mapema wiki hii baada ya waandishi wa habari hizi kutaka kujua muamko wa wananchi katika kushiriki michakato hiyo.

Wakati hali hiyo ikijitokeza kwa wananchi kwa upande wa  viongozi wa serikali za mitaa Chanika Wilayani Ilala wamesema kuwa wananchi wao bado hawajapata elimu ya kutosha kuhusu mambo hayo matatu yakitaifa yanayofanywa kwa wakati mmoja.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa mtaa wa Nyeburu Chanika Manispaa ya Ilala Bw.Kassimu Uchuro alisema kuna haja mamlaka zinazohusika kutoa elimu ya kutosha kwa viongozi wa serikali za mitaa ili na wenyewe waweze kuwapa elimu hiyo wananchi ya kutambua umuhimu wa kushiriki michakato hiyo.

"Unajua wananchi bado hawajapa elimu kuhusu michakato hii kama unavyojua mwaka huu kuna mambo takribani matatu yanafanyika kwa wakati mmoja ,sasa kunakuwa na muingiliano wa utekelezaji wake hivyo watalaamu hawa waje kutoa elimu kwetu ili nasi tuweze kuwaelimisha wananchi wetu juu ya suala zima la sensa na vitambulisho vya Taifa pamoja na mchakato wa katiba mpya,"alisema

Alisema kuwa changamoto zinazojitokeza kwa sasa ni suala zima la waislamu kukataa kujiandikisha katika sensa na kulifanya suala hilo kuliingiza katika vitambulisho vya utaifa.

Kwa upande wa Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Matumbi Temeke ambaye pia ni Mwenyekiti wa wenyeviti wote wa Temeke, Bw. Othumani Omari alisema kuwa kwaupande wake zoezi hilo linaenda vizuri,kwakuwa wanachi wamepata elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kujiandikisha ili kupata vitambulisho vya utaifa.

Naye Mwenyekiti wa Keko B, Bw. Philipo Maganga alisema kuwa kutokana na elimu ambayo wameipata vijana kuandikisha wananchi zoezi hilo linakwenda vizuri kwakusaidiana na mabalozi wa nyumba kumi.

No comments:

Post a Comment